HabariSiasa

Hatuna ripoti za njama ya kuua Ruto – Kibicho

July 9th, 2019 1 min read

Na AGEWA MAGUT

KATIBU wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho amepuuzilia mbali madai kwamba anahusika na njama ya kumuua Naibu Rais William Ruto.

Akiongea na wanahabari Jumatatu baada ya kuzindua kisima cha maji katika kambi ya Polisi wa Utawala (AP) ya Shauri Moyo jijini Nairobi, Bw Kibicho alisema madai hayo hayajaripotiwa rasmi kwa ofisi husika za usalama.

“Siko tayari kujibu madai yasiyo na msingi kwa sababu yanachunguzwa na polisi. Tuna habari za kijasusi, tuna akili bora kuliko yale mnayoyasikia lakini kwa bahati mbaya siwezi kutumia vyombo vya habari kuzungumzia mambo ya kubuni,” Dkt Kibicho akasema.

Alieleza kuwa hakuna malalamishi rasmi ambayo yamewasilishwa popote kumhusisha na madai hayo.

“Nasikia madai ya mauaji. Nani amelalamika? Sijasikia kwamba mtu yeyote amelalamika. Nadhani ni bora wakome kubuni mambo ambayo hayapo. Madai ambayo yanatolewa kwenye mikutano hayana msingi wowote hadi pale yatakapothibitishwa kwa mujibu wa sheria,” Dkt Kibicho akaeleza.

Katibu huyo pia alikosoa ripoti iliyotolewa na Shirika la Human Rights Watch (HRW) kuhusu madai ya kukithiri kwa visa vya mauaji ya kiholela ya washukiwa wa uhalifu yanayodaiwa kutekelezwa na maafisa wa usalama nchini.

Dkt Kibicho aliwataka wananchi kuwapa nafasi maafisa wa polisi watekeleze majukumu yao ya kuchunguza visa vya uhalifu.

Ripoti hiyo ya HRW ilidai kuwa polisi wamehusika katika mauaji ya washukiwa 21 katika mitaa miwili ya Nairobi tangu Agosti mwaka jana.

Dkt Kibicho alikuwa ameadamana na Katibu wa Wizara ya Maji, Joseph Irungu wakati wa uzinduzi wa kisima hicho.