Habari MsetoSiasa

Hatuna uwezo wa kukabili corona – Magavana

April 2nd, 2020 2 min read

Na PATRICK LANG’AT

BARAZA la Magavana limekiri kwamba kaunti zote haziko tayari kukabiliana na janga la corona ikiwa hali itazidi kuwa mbaya siku zinazokuja.

Idadi ya maambukizi inaendelea kuongezeka nchini, na serikali ilionya huenda watu 10,000 wakaambukizwa kufikia mwisho wa Aprili.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (COG), Wycliffe Oparanya, alisema hali ikidorora zaidi na kila kitu kisimamishwe nchini, ni kaunti za Nairobi na Mombasa pekee zinazoweza kukabiliana na hali kama hiyo.

“Tunafaa kujiuliza wenyewe, iwapo kila kitu kitasimamishwa: Tuna chakula cha kutosha? Je, uchumi wetu unaweza kuhimili hali hiyo? Sioni jinsi serikali ya kitaifa inaweza kufanikisha amri hiyo isipokuwa waitangaze Nairobi na Mombasa pekee,” alisema Bw Oparanya akihutubia wanahabari katika afisi yake iliyoko Delta House, Nairobi.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ameshauri Wakenya kujitenga na maeneo ya watu wengi na kutii amri ya kutotoka nje usiku kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na moja asubuhi kuepuka kusambaa kwa virusi hivyo nchini.

“Siwezi kusimama hapa na kusema kwamba tumejiandaa kwa asilimia mia moja. Iwapo, kama ilivyokuwa Italia, tuna watu 600, 800 wanaokufa kila siku, tutakuwa na shida ya kupata hata mbao za kutengeneza majeneza,” alisema Bw Oparanya.

Kaunti zina uhaba wa maji ya mifereji yanayotiririka kila wakati, hitaji muhimu kukabili corona kwa kunawa mikono mara nyingi iwezekanavyo.

Kwenye mkutano wa jana na wanahabari, Bw Oparanya alisema kaunti zinang’ang’ana kutimiza mahitaji mengine kama vile vitanda maalumu vya wagonjwa.

“Hatuna uwezo wa kujenga hospitali kwa wiki moja kama China ilivyofanya. Kwa hivyo, vituo vyetu vya kutenga wagonjwa vitakuwa katika shule za mabweni,” alisema Bw Oparanya. Kuhusu vifaa vya kujikinga, mwenyekiti huyo alisema serikali za kaunti zinatatizika kupata vilivyo bora.

“Katika kaunti ya Kakamega, ninafaa kuwa na 1,000 lakini niko na 300. Siwezi kuvipata sokoni, na hata nikipata, siwezi kuhakikisha ubora wake,” alisema na kuomba Wizara ya Afya kuwapa ubora unaotakiwa ili waweze kuvinunua kwa kutegemea bajeti ya kila kaunti.

Kwa serikali za kaunti kujiandaa kwa corona ni jambo lisiloweza kuepukika, hasa baada ya serikali ya kitaifa kusema visa vya maambukizi vinatarajiwa kufika 10,000 mwishoni mwa Aprili.

Bajeti ya serikali za kaunti ni ndogo na ikizingatiwa kasi ya maambukizi, zimelazimika kubadilisha majengo yaliyokuwa yametelekezwa, wadi ambazo hazikuwa zikitumiwa na wadi mpya za kujifungulia akina mama kuwa za kutenga wagonjwa wa corona.

Kwa mara nyingine, Bw Oparanya aliwahimiza Wakenya wanaoishi jijini Nairobi kutosafiri mashambani akisema wanahatarisha maisha ya wazee wanaoishi vijijini.

“Ni vigumu kuchukua hatua za kuzuia watu kusafiri kwenda mashambani kutoka Nairobi. Kwa hivyo, tunatoa ombi kwa wote kuwahimiza: Kaa uliko. Usiende mashambani kwa sababu wazee watakuwa hatarini,” alisema.

Baraza la Magavana limemteua gavana wa Kisumu na Afisa Mkuu Jackline Mogeni kuungana na mwenyekiti wa kamati ya afya katika kamati ya kukabiliana na corona inayosimamiwa na Waziri Kagwe.