Michezo

Hatuogopi yeyote katika kampeni za Afcon '19 – Kahata

June 18th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

ZIKISALIA siku tatu kindumbwendumbwe cha Kombe la Afrika (AFCON) kianze nchini Misri, Francis Kahata amesema Harambee Stars haina uoga inapojiandaa kufungua kampeni dhidi ya Algeria hapo Juni 23 jijini Cairo.

Katika mahojiano na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) katika kambi ya mazoezi ya Stars jijini Paris nchini Ufaransa, kiungo huyo matata wa Gor Mahia aliongeza kwamba timu iko tayari kwa kibarua hicho.

“Sidhani kuna mtu aliye na uoga timuni. Tumepata uzoefu kwa kushiriki mashindano ya Afrika ya klabu na kukutana na wachezaji wazuri barani humu. Mechi za ligi mbalimbali duniani na zile za kimataifa za kirafiki pia zimetusaidia kupata uzoefu. Naamini mafunzo hayo yatatufaa zaidi katika AFCON,” alisema kiungo huyu wa Gor Mahia anayemezea mate na miamba wa Tanzania, Simba SC.

Aidha, wapinzani wa Kenya kwenye mechi za makundi za AFCON Senegal, Algeria na Tanzania walikamilisha mechi zao za kirafiki Jumapili.

Nyota wa Algeria, Riyad Mahrez ameonya Kenya inayonolewa na Sebastien Migne ijiandae kwa mchuano mkali.

Teranga Lions ya Senegal iliuma Super Eagles ya Nigeria 1-0 kupitia bao la kiungo wa Everton Idrissa Gueye mjini Ismailia nchini Misri, Desert Foxes ya Algeria ikang’ata Mali 3-2 baada ya kutoka chini mara mbili mjini Doha nchini Qatar nayo Tanzania ikakaba Zimbabwe 1-1 jijini Cairo mnamo Jumapili.

Timu zote nne kwenye Kundi C zilisakata mechi mbili za kirafiki ambapo Kenya ilifagilia mbali Madagascar 1-0 jijini Paris nchini Ufaransa mnamo Juni 7 na kutupa uongozi dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi iliyotamatika 1-1 jijini Madrid nchini Uhispania.

Algeria ilikabwa 1-1 dhidi ya Burundi mnamo Juni 11, Tanzania ikachapwa 1-0 na wenyeji Misri mnamo Juni 13 nao Senegal wakalemea klabu ya Real Murcia 7-0 nchini Uhispania na Super Eagles ya Nigeria 1-0.

Algeria ilikita kambi katika joto la Qatar inaamini iko tayari sio tu kuanza mashindano, bali pia kuzoa alama tatu dhidi ya Stars iliyofanyia mazoezi katika mazingira ya baridi nchini Ufaransa.

Mahrez, ambaye amesifiwa na kocha Djamel Belmadi kwa kufanya kazi yake ya kumega pasi za uhakika za kuzalisha magoli na pia kufunga baada ya kuchezeshwa kama mchezaji wa akiba, alisema, “Tumekuwa na vipindi vya kufana vya mazoezi na katika joto kali linalopatikana Misri kwa hivyo hatutakuwa na vijisababu vyovyote dhidi ya Kenya. Tuko tayari kwa AFCON.”

Belmadi alisema ushindi dhidi ya Mali ni motisha kabla ya kukabili Kenya.

“Tulipata upinzani mzuri dhidi ya Mali ambayo mchezo wake unakaribiana sana na wa Senegal. Mali imecheza pamoja kwa muda mrefu katika mashindano ya Afrika na Kombe la Dunia ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20. Kwa jumla, tulikuwa hatari na kuunda nafasi nyingi nzuri ambazo hatukuzitumia vyema…  Tunachojutia ni kufungwa mabao mawili hasa kutokana na ikabu – penalti na kona, na tutahitajika kurekebisha. Tuna makali ya kuzamisha Kenya,” alinukuliwa akisema.