Habari za Kitaifa

Hatutabeba mtu yeyote mpaka wenzetu waachiliwe, bodaboda wa Kitengela wasema

January 22nd, 2024 1 min read

Na STANLEY NGOTHO

TAKRIBAN wahudumu 1,500 wa bodaboda katika mji wa Kitengela Jumatatu asubuhi walisitisha huduma zao wakilalamikia kukamatwa kwa wenzao kufuatia tukio la Alhamisi ambapo bodaboda walinaswa kwenye video wakishambulia na kupiga mawe mwendesha gari.

Inadaiwa mwendeshaji huyo alisababisha ajali iliyoishia kwa maafa ya mwanabodaboda mmoja.

Wahudumu hao wanasema polisi kwa siku tatu zilizopita wamekuwa wakikamata wahudumu licha ya kiongozi wao kukubali kusaidia kutambua wahusika.

Soma pia Wizi wa pikipiki wazidi wahudumu wakiuawa

Halafu Kizaazaa Mama Mboga akidunga kisu ng’ombe aliyejaribu kula bidhaa zake sokoni

Kisha Mwanafunzi aliyesaidiwa na shirika la Nation Media kupata ufadhili afaulu kuzoa alama A

Jumatatu asubuhi, walisusia mkutano ulioandaliwa na polisi na maafisa wa utawala kabla ya kuegesha pikipiki zao na kukataa kutoa huduma. Walibeba mabango wakikashifu polisi kwa unyanyasaji.

Pikipiki zote ziliegeshwa na kusababisha matatizo makubwa ya uchukuzi katika mji huo wenye shughuli nyingi. Waendeshaji ambao walijaribu kurejelea shughuli waliondolewa kwa nguvu kutoka kwa barabara, halafu pikipiki zote zikaegeshwa katika na afisi za Naibu Kamishna wa Kaunti.

“Hatuungi mkono kile kisa cha kupigwa mawe kwa dereva wa gari lakini hatutakubali tukio hilo litumiwe na maafisa wa usalama kutunyanyasa. Kuna baadhi ya wahudumu ambao hawana hatia ilhali wamekamatwa. Hatutarejelea shughuli mpaka waachiliwe,” akasema John Musau, mwanabodaboda.

Wanataka wenzao waachiliwe wakisema wako tayari kutambua wahuni waliohusika na kitendo  cha Alhamisi.