Makala

Hatutaki maneno matupu: Wakulima Nyeri wataka Kenya Kwanza iwape hazina ya mazao waliyowaahidi

January 13th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

WAKULIMA wa kahawa katika Kaunti ya Nyeri sasa wanamtaka Rais William Ruto kutekeleza Mpango wa Kuboresha Bei za Mazao yao (GMR) haraka, kama alivyowaahidi wakati wa kampeni za mrengo wa Kenya Kwanza mnamo 2022.

Wakiwa pamoja na viongozi tofauti kutoka eneo hilo, wakulima hao walisema wakati umefika kwa utawala wa Kenya Kwanza kutekeleza ahadi hiyo, kama njia ya kuwarudishia mkono kwa kuupigia kura kwa wingi.

“Kama wakulima, tulijitokeza kwa wingi kuupigia kura utawala huu. Hata hivyo, nina masikitiko makubwa,” akasema Bw Martin Muthee, ambaye ni mkulima.

Akaongeza: “Mlituahidi kutekeleza mfumo wa GMR kwa mazao yetu. Sasa tunasikia mnataka kutulipa malipo yetu ya kahawa kwa awamu. Tunataka kujua wakati ahadi hii itaanza kutekelezwa.”

Kauli yake iliungwa mkomo na mbunge wa Mathira, Eric Wamumbi, aliyesema kuwa mfumo huo unafaa kutekelezwa mara moja ili kuwasaidia wakulima kulipa madeni yao.

“Wakulima hawa wanataka hakikisho la kuboreshwa kwa mazao yao. Pia, wanataka kuondolewa madeni waliyo nayo. Hii ndiyo njia pekee ya kuwatuliza,” akasema Bw Wamumbi.

Mwakilishi wa Kike wa kaunti hiyo, Bi Rahab Mukami, alieleza kuwa madeni ya wakulima hao yanafaa kufutiliwa mbali kama yale ya wakulima wa miwa.

“Imekuwa vigumu kwa wakulima kutoka eneo hili kulipa madeni yao. Nilikuwa pamoja na Rais wakati madeni ya wakulima wa miwa yalifutiliwa mbali; tunahitaji hatua kama hiyo kuchukuliwa katika sekta ya kahawa ili kuifufua tena sekta hiyo,” akasema Bi Mukami.

Seneta Wahome wa Matinga, kwa upande wake, alisema kuwa fedha zilizotengewa Hazina Maalum ya Kahawa zinafaa kuongezwa kutoka Sh6.7 milioni hadi Sh12 milioni.

“Kama serikali, tunafaa kuongeza fedha zilizotengewa hazina hiyo ili kuhakikisha wakulima wananunuliwa zao hilo vizuri, hata wakati bei yake iko chini. Mabadiliko ya kimsimu hayafai kuwafanya kuteseka,” akasema seneta huyo.

Mbunge John Kagucia (Mukurwe-ini) pia alitoa kauli kama hiyo.

Wakulima walimkasirikia Waziri wa Mashirika, Simon Chelugui, alipopendekeza kuwa watalipwa malipo yao ya kahawa kwa awamu mbili.

Hata hivyo, waziri alisema serikali itaangalia vile itawalipa wakulima hao kwa awamu moja.

Kwa sasa, serikali inanunua kilo moja ya kahawa kwa Sh80 kiwastani.