Kimataifa

Hatutaki msaada wa kigeni kusaka bilionea, TZ yasema

October 18th, 2018 2 min read

Na MASHIRIKA

TANZANIA imesema haitaomba mashirika ya kigeni kusaidia kumtafuta bilionea Mohammed Dewji aliyetekwa nyara wiki iliyopita.

Waziri msaidizi wa mashauri ya ndani wa nchi hiyo, Hamad Masauni alinukuliwa akisema kwamba hakuna mipango ya kualika wachunguzi wa kigeni upinzani ulivyotaka.

Viongozi wa upinzani wamekuwa wakilaumu serikali kwa kujivuta kumsaka Dewji na kudai huenda ilihusika na kutekwa nyara kwake.

Bw Masauni alisema kualika wachunguzi wa kigeni ni sawa na kuamini wale wanaodai kwamba serikali ilihusika na utekaji nyara wa bilionea huyo mchanga zaidi barani Afrika.

Dewji, 43, alitekwa na watu waliokuwa na bunduki alipokuwa akiingia chumba cha mazoezi ya viungo vya mwili jijini Dar es Salaam.

Polisi walisema hakuwa na walinzi wakati wa kisa hicho cha Alhamisi asubuhi.

Ripoti za polisi zilisema kwamba watu 20 walikamatwa kwa kushukiwa kuhusika na kisa hicho lakini hakukuwa na habari za kule aliko.

Awali, polisi walihusisha utekaji nyara huo na raia wa kigeni wazungu lakini walioshuhudia walisema waliona watu watatu waliofunika nyuso zao.

Mnamo Jumatatu, familia ya Dewji ilitoa zawadi ya Sh44 milioni kwa atakayetoa habari zitakazosaidia kumpata.

“Sisi familia ya Dewji tunataka kuhakikishia yeyote aliye na habari kuhusu aliko mwana wetu ajitokeze na tutaweka siri habari hizo,” alisema Azim Dewji, mjomba wa bilionea huyo.

Dewji anamiliki kampuni za MeTL Group zinazopatikana katika nchi 10 ulimwenguni ambazo zinahusika na kilimo, bima, uchukuzi na chakula.

Kati ya 2005 na 2015, alihudumu kama mbunge na 2013 alikuwa raia wa kwanza wa Tanzania kuangaziwa na jarida Forbes. Miaka miwili baadaye alishinda tuzo za Forbes’ Africa Person of the Year.

Mfanyabiashara huyo alikuwa mwenye hisa katika kilabu ya soka ya Dewji nchini Tanzania.

Jana, polisi walisema kamera za usalama katika hoteli ya Colosseum ambazo zingewasaidia kutambua watekaji nyara hazikuwa zikifanya kazi.

Kauli hii ni tofauti na iliyotolewa awali na kamanda wa polisi eneo la Dar es Salaam, Paul Makonda na mkuu wa kikosi maalumu Lazaro Mambosasa ambao waliambia wanahabari kwamba kamera hizi zilionyesha watekaji nyara walikuwa wakiendesha gari aina ya Toyota Surf.

Japo Bw Mambosasa alisema kamera hizo hazikuweza kuonyesha kilichotendeka, uchunguzi wa gazeti la Mwananchi ulionyesha maeneo mengi ya barabara ya Haile Selassie yamewekwa kamera zenye nguvu.

Ramadhani Juma anayefahamika kama P Square, ambaye ni mhudumu katika hoteli ya Coco Beach, Dar es Salaam, alisema alitekwa nyara Juni mwaka huu na kuachiliwa baada ya wiki moja.

“Nilitekwa siku ya Idd. Ilikuwa Alhamisi jioni na watu waliokuwa na gari walionipeleka eneo ambalo sikutambua wakanitesa. Nilipiga duru lakini hakuna aliyenisaidia na waliendelea kunipiga wakiniwekelea bunduki na kunilaumu kuwa jambazi,” aliambia gazeti The Citizen.