Siasa

Hatutaki serikali jumuishi, wandani wa Gachagua Mlima Kenya wafokea Ruto

Na MWANGI MUIRURI August 13th, 2024 2 min read

BAADHI ya wanasiasa wa Mlima Kenya wamemchemkia Rais William Ruto kwa kuwashirikisha wandani wa Raila Odinga katika serikali yake, wakisema hatua hiyo inakandamiza demokrasia.    

Wandani sita wa Bw Odinga waliteuliwa katika Baraza la Mawaziri ambalo lilitangazwa na Rais Ruto mwezi uliopita, Julai 2024, kutuliza maandamano ya Gen Z.

Ukanda wa Mlima Kenya ulimpa Rais asilimia 87 ya kura 2022 na baadhi ya wanasiasa kutoka eneo hilo sasa wanasema nafasi ambazo wandani wa Raila walipewa zingeishia mlimani.

Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara alisema eneo hilo haliungi mkono serikali jumuishi akisema hakuna haja ya kufanyika kwa uchaguzi kila mara kisha Raila anapitia mlango wa nyuma na kuingia serikalini.

“Hatua ya Rais kuleta watu wa ODM ndani ya serikali haifai na inafanya kura ya Wanjiku isiwe na umuhimu wowote. Hii inaonyesha kuwa nchi hii ina wenyewe wawe wamepigiwa kura au la,” akasema Bi Kihara ambaye ni mwandani wa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Naibu Rais mwenyewe akiwa Mlima Kenya wikendi alisema wafuasi wake hawana shida na serikali jumuishi na akasema watawaonyesha wandani wa Raila jinsi ya kufanya kazi.

Bi Kihara alienda hatua zaidi akisema kuwa uchaguzi unastahili kupigwa marufuku kisha wazee wa kieneo wapewe jukumu la kukutana na kuamua Rais na baraza la mawaziri.

Alisema wawaniaji hutumia pesa nyingi wakati wa kura na hupitia msongo wa mawazo baada ya kupoteza.

“Kuja baadaye na kubatilisha uamuzi wa raia ni siasa mbaya. Rais ni mwanasiasa na sasa anatufanyia hivi kwa sababu analenga siasa za 2027,” akaongeza Bi Kihara.

Mbunge huyo wa Naivasha alisema hakukuwa na haja ya Rais kuwaendea wanasiasa wa upinzani ilhali ODM ililemewa katika kura ya 2022.

Vilevile, alimhusisha Rais na makabaliano ya kisiasa ambayo yamekuwa yakimzingira Bw Gachagua ikiwemo wandani wake kuandamwa na vyombo vya usalama.

“Yeye ndiye amekuwa akiongoza mikutano ya kumpinga Gachagua. Wandani wa Gachagua hawajakuwa wakialikwa katika mikutano hiyo na kuna moja ambayo walinialika kimakosa na nilipofika waliharakisha mambo na kumaliza,” akasema Bi Kihara.

Mbunge huyo wa UDA alishutumu ziara ya wiki jana ya Rais Mlima Kenya akisema kuwa ilikuwa tu ya kupigia upatu baraza jipya la mawaziri ambalo linaridhisha Bw Odinga.

Aliyekuwa mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri pia alisema baraza jipya la mawaziri linaonyesha tu kuwa Rais amewasaliti wakazi wa Mlima Kenya waliompigia kura.

“Tumeonyeshwa kuwa kura zetu hazina umuhimu kwa sababu ni wanasiasa wawili ndio wanaamua uongozi wa nchi. Tuondoke katika serikali hii, tuunde chama chetu cha Mlima Kenya kisha tuwanie Urais 2027.

“Tukishinda au kupoteza kwenye uchaguzi huo bado tutaishia kwenye serikali ya muungano jinsi Raila anavyofanya baada ya kila uchaguzi,” akasema Bw Ngunjiri.

Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, ambaye ni mwandani wa Bw Gachagua amenukuliwa hapo awali akisema kuwa wanafuatilia matukio ya kisiasa na kuona iwapo maslahi ya Mlima Kenya yataendelea kulindwa na utawala huu.