Hatutakubali utupange, Ruto aambia Uhuru

Hatutakubali utupange, Ruto aambia Uhuru

Na SIAGO CECE

NAIBU Rais William Ruto jana Jumamosi aliongoza washirika wake katika muungano wa Kenya Kwanza Alliance kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuacha siasa za kuamua atakayemrithi.

Akizungumza akiwa kaunti ya Kwale, Dkt Ruto alisema Rais Kenyatta anamuunga kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kupitia Azimio la Umoja, ili aweze kuendelea kutawala kupitia njia mkato hata baada ya kuondoka mamlakani.

Dkt Ruto aliyeandamana na kiongozi wa Amani National Congress Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula walisema mkutano wa Rais Kenyatta na wabunge wa Jubilee katika Ikulu ya Nairobi Ijumaa aliposemekana aliidhinisha Azimio la Umoja ni dhihirisho kwamba Bw Odinga ni mradi wake.

“Tunajua njama ya Rais ya kuchagua mtu anayetaka na kuendelea kutawala serikali jambo ambalo hatutakubali. Wanachagua mtu atakayelinda maslahi na matakwa yao pekee,” alisema Dkt Ruto.

Bw Mudavadi alisema hatimaye Rais Kenyatta amefichua kwamba Azimio la Umoja ni mradi wake.

“Tumegundua kwamba Rais Uhuru Kenyatta ndiye mwenye Azimio la Umoja. Bw Odinga ni mradi wa Rais Kenyatta na wanakata mwanachama wa Jubilee kuwa mgombea mwenza wa mradi huo,” alisema Bw Mudavadi.

Viongozi hao walisema Wakenya wanafaa kuachwa wachague wanaotaka wawaongoze kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu.

“Kutaka kulazimishia Wakenya anatakayekuwa Rais na Naibu Rais wa nchi ni hatari kwa nchi,” alisema Bw Wetang’ula.

Walimtaka Rais Kenyatta kujitenga na siasa za urithi.

“Tunakabiliwa na hatari ya muhula wa tatu wa Rais Kenyatta iwapo Azimio itashinda urais na hii itakuwa ni sawa na kupindua katiba,” alisema seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.

You can share this post!

Jubilee, ODM kuonyesha Ruto ubabe

Mvurya adai mgomo wa madaktari umechochewa kisiasa

T L