Hatutambui mkataba wa kusitisha vita – M23

Hatutambui mkataba wa kusitisha vita – M23

KINSHASA, DRC

KUNDI la waasi la M23 limesema tangazo kuhusu kusitishwa kwa vita lililotolewa wiki hii haliwahusu huku likiitisha mazungumzo ya moja kwa moja kati yake na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“M23 imeona stakabadhi hiyo katika mitandao ya kijamii… Hakukuwa na mtu yeyote katika mkutano huo wa viongozi (kutoka M23) kwa hivyo hautuhusu kwa njia yoyote,” Lawrence Kanyuka, ambaye ni msemaji wa kisiasa wa vuguvugu la M23 akasema.

“Kawaida makubaliano ya kusitishwa kwa vita huwa yanahusu pande mbili kwenye mapigano,” akaongeza.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Rwanda Vincent Biruta walihudhuria mkutano huo uliofanyika Angola mnamo Jumatano.

Kwenye kikao na wanahabari jijii Kinshasa mnamo Alhamisi jioni, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa DRC Christopher Lutundula alisema: “Kesho saa kumi na mbili jioni (6:00pm), M23 sharti isitishe mashambulio yake yote.”

Waasi wa M23 wamekuwa wakitulia kwa miaka kadhaa, lakini walianza vita tena mwishoni mwa mwaka 2021.

Serikali ya DRC imedai kundi hilo la wapiganaji linasaidiwa na Rwanda, lakini taifa hilo jirani limekana madai hayo.

Juzi, waasi hao waliteka sehemu kubwa ya Kaskazini mwa Goma, ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

Mkutano uliofanyika jijini Luanda, Angola ulifikia makubaliano kwamba vita mashariki kwa DRC visitishwe kuanzia jana Ijumaa jioni.

Baada ya kusitishwa kwa vita hivyo waasi wa M23 waondoke maeneo ambayo wameteka na warejee katika vituo vyao vya zamani.

Wajumbe katika mkutano huo walikubaliana kwamba endapo waasi hao watakataa kusitisha vita na kuondoka maeneo waliyoteka vikosi vya wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) watatumia nguvu kuwafurusha.Kanyuka alisema waasi walitangaza “kusitisha vita” mnamo Aprili na waliamini kwamba hawajarejelea vita.

“Ikwa kufikia kesho (jana Ijumaa) saa kumi na mbili jioni au asubuhi siku itakayofuata, serikali haitakuwa imetushambulia, bado tutakuwa hapo,” akasema.

Hata hivyo, “tutajilinda sisi wenyewe,” Kanyuka akasema.

“Kila mara huwa tuko tayari kwa mazungumzo na serikali ya DRC kushughulikia chanzo cha mapigano,” akaongeza.

Lakini serikali ya Rais Tshisekedi imekataa kufanya mazungumzo na kundi la M23, ambalo imelitaja kama “kundi la kigaidi” mradi linaendelea kudhibiti maeneo mbalimbali nchini DRC.

Akijibu swali kutoka kwa mwanahabari mmoja, Waziri Lutundula alikatalia mbali uwezekano wa serikali ya nchi hiyo kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la M23.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano wa Angola, ulioongozwa na Rais wa nchini hiyo Joao Lourenco, walikuwa ni; Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye na mjumbe wa amani wa EAC, Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uingereza na Amerika waambulia...

Gachagua, Mudavadi wajipanga kwa 2027

T L