Michezo

Hatuwaogopi hao Kariobangi Sharks – KCB

February 7th, 2020 1 min read

JEFF KINYANJUI na JOHN ASHIHUNDU

KOCHA Zedekiah Otieno ‘Zico’ leo Ijumaa alasiri ana kibarua kigumu kuongoza kikosi chake cha Kenya Commercial Bank (KCB) dhidi ya Kariobangi Sharks katika mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) itakayochezewa Kenyatta Stadium mjini Machakos.

Ni mtihani mkubwa dhidi ya Sharks ambao majuzi waliibuka na ushindi mkubwa wa 8-1 dhidi ya Kisumu All Stars, lakini Otieno anasema vijana wake wako tayari kwa kibarua hicho.

“Huwezi kutulinganisha na Kisumu All Stars, kwa sababu wako katika nafasi mbaya jedwalini, wakati sisi tukiwa miongoni mwa tano bora. Tumejiandaa vyema kwa mechi hii na lengo letu ni kupata pointi zote tatu,” akasema Otieno.

Akaongeza: “Nashukuru Mungu hatuna majeraha yoyote kwa sasa na kila mtu anasubiri kwa hamu mechi ya kesho (leo Ijumaa) baada ya maandalizi ya kutosha. Nafurahia jinsi mambo yanavyoenda kwa sasa.”