Kimataifa

Hatuwataki wazee, vijana waambia Trump na Biden uchaguzi ukinukia

May 16th, 2024 2 min read

WASHINGTON DC, AMERIKA

IDADI kubwa ya wapigakura ambao ni vijana katika uchaguzi wa urais nchini Marekani wanasema wanatamani kupata mgombeaji mwingine wala sio Joe Biden na Donald Trump.

Katika uchaguzi mkuu unaoratibiwa kufanyika Novemba mwaka huu, kinyang’anyiro kitakuwa kati ya wagombeaji hao wawili kutoka vyama viwili vikubwa.

Hata hivyo, kukiwa na maswali katika kampeni kuhusu afya ya wagombeaji hao, suala la nguvu za anayeshikilia madaraka limeibuka.

Kulingana na kura ya maoni ya Shirika la wa Pew Research wiki iliyopita, thuluthi mbili ya wapigakura ni chini ya umri wa miaka 30 na huenda wasiwatake wagombeaji hao wakuu iwapo watapata fursa.

Mpigakura, Desmond Kager, kutoka jimbo la New Hampshire aliomba vyama hivyo viwili, Democratic cha Biden na Republican cha Trump, vichangue wagombeaji wengine.

“Kama Warepublican na Wademocrat, unajua, muweke mtu mwingine kwenye tiketi ya urais, unafahamu, ni vizuri kupiga kura, halafu nitawapigia kura,” alisema Bw Kager.

Mbali na umri msukumo wa vijana kumtafuta mwaniaji mwingine limejikita katika suala la uzazi. Mpigakura Francesca Panniello, akiwa na wasiwasi kuhusiana na haki ya uzazi inayoungwa mkono na Rais Biden.

“Ninadhani kutoa mimba, kutoa mimba ni muhimu kwangu. Huduma katika utoaji mimba, haki ya kuwa na uwezo wa kuchagua,” aliongeza Panniello.

Kulingana na chama cha Democratic, kikitumia njia ya kuwapigia simu wapigakura ambao ni vijana, haki ya utoaji mimba na bangi ya burudani ulijitokeza.

Kwenye upigaji kura huo wa maoni, baadhi ya vijana wanampinga Biden kwa kuunga mkono Israeli katika vita ukanda wa Gaza.
Bi Eliana Stein, mpigakura kutoka Massachusetts alieleza huenda akapata kura yake.

“Ninahisi kama hivi sasa, kwangu mimi, jambo moja muhimu sana ni kuendelea kuunga Israeli, hasa wakati wote wa mzozo ambao unaendelea. Kwa kweli ninashukuru kila kitu ambacho Rais Biden amefanya kuiunga mkono Israeli katika mzozo wa sasa,” alieleza Bi Stein.

Utafiti huo ulionyesha kuwa wengi wa vijana wanaomuunga mkono Trump, wana mazoea ya kutembelea maeneo ya burudani.

Mnamo Machi 2024, ukusanyaji wa maoni ya mashirika ya Reuters na Ipsos ulionyesha kuwa wananchi wa Amerika walio na umri kati ya miaka 18 na 29 wanampendelea Biden dhidi ya Trump kwa asilimia tatu.

Hiyo ni idadi ndogo kuliko mwanya wa asilimia 24 ambao Biden alishinda kura ya vijana miaka minne iliyopita.