Habari Mseto

Hatuwezi kuchapisha lebo feki za KEBS, Madras yajitetea

July 9th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMPUNI inayochapisha lebo ambazo hutumiwa na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs) kuidhinisha ubora wa bidhaa zinazoingizwa humu nchini imepinga madai kuwa inashiriki katika sakata ya uchapishaji lebo feki.

Kwenye taarifa iliyochapishwa magazetini jana Madras Security Printers (MSP) kampuni hiyo ilisema haijawahi kupokea malalamishi yoyote kutoka kwa Kebs au shirika lolote la serikali kwamba baadhi ya lebo zake si halali.

“Madai kwamba MSP huchapisha lebo (Import Standardization Mark –ISM) feki ambazo hutumiwa kufanikisha uingizwaji wa bidhaa ghushi nchini hayana ukweli wowote. ISMs ambazo zimekuwa zikiwasilishwa kwa Kebs zimekuwa zikiafikia masharti ya kiusalama yaliyomo kwenye zabuni… kwa hivyo tunashangaa kusikia madai hayo dhidi yetu,” ikasema taarifa hiyo ambayo haikutiwa saini na wakuu wa kampuni hiyo kutoka India.

Kulingana na kampuni hiyo lebo hizo hutengenezwa katumia mashine za kisasa huku suala la usalama likipewa uzito mkubwa.

“Muhimu zaidi ni kwamba lebo hizo za kutumiwa na Kebs hutengenezwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa ambavyo hutumika katika vita dhidi ya bidhaa feki,” taarifa hiyo inaeleza.

Mwezi jana, maafisa wa upelelezi walifichua sakata ambapo maafisa wa Kebs wamekuwa wakishirikiana na wale wa kampuni ya Madras Security Printers kuchapisha lebo feki za ubora.

Mkurugenzi wa Upelelezi a Jinai (DCI) George Kinoti alisema maafisa wake walibaini kuwa lebo hizo feki huchapishwa katika afisi za Kebs humu nchini.

“Hizi lebo hazitengenezwi katika barabara ya Kirinyaga; zinatengenezwa maeneo fulani katika afisi za Kebs. Bila shaka tutawashtaki watu fulani kuhusiana na sakata hii,” akasema katika makao makuu ya DCI Nairobi baada ya maafisa wake kunasa sukari ya magendo mtaani Eastleigh.

Lebo hizo, wakisema, ndizo hutumiwa na wafanyabiashara walaghai ambao huingiza bidhaa za magendo pamoja na watengenezaji wa bidhaa feki. Kando na sukari, lebo hizo hutumika kuidhinisha bidhaa, kama vile, juisi, mafuta ya kupikia, mbolea na betri ghushi ambazo huingizwa nchini kimagendo, zingine zikiwa hatari kwa afya ya mwanadamu.

Mkurugenzi wa Kebs aliyeshtakiwa Charles Ongwae alikana madai hayo lakini Mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo Mugambi Imanyara alikubali uwepo wa sakata hiyo.

“Kuna idadi kubwa ya lebo feki za ubora ya bidhaa kiasi kwamba hatuwezi kutofautisha kati ya bidhaa hali na zile feki au la,” akasema Bw Imanyara.