Michezo

Hatuwezi kumuuza Harry Kane kwa mpinzani wetu EPL – Spurs

April 20th, 2020 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

TOTTENHAM Hotspur wameshikilia kuwa hawana nia ya kuzinadi huduma za mvamizi na nahodha wao Harry Kane msimu huu.

Aidha, wamefichua kwamba muda wa kumtia mnadani sogora huyo mzawa wa Uingereza utakapowadia, hawatakuwa radhi kumuuza kwa mpinzani wao yeyote katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kane mwenye umri wa miaka 26 angali na muda wa miaka minne katika mkataba mpya wa miaka sita aliotia saini kambini mwa Tottenham mnamo Juni 2018.

Mwezi jana, Kane ambaye amekuwa tegemeo kubwa katika kikosi cha Tottenham alisema kwamba hayuko tayari kuendelea kuhudumu kambini mwa waajiri wake hao bila ya kujitwalia mataji ya haiba kubwa zaidi yakayomkuza kitaaluma.

Kauli hiyo ilimchochea Daniel Levy ambaye ni mwenyekiti wa Tottenham kudokeza uwezekano wa kumuuza Kane mwishoni mwa muhula huu kwa kima cha Sh28 bilioni.

Ingawa Manchester United ni miongoni mwa vikosi ambavyo vimekuwa vikihemea maarifa ya Kane, huenda bei ya nyota huyo ikawakunjisha mkia na hivyo kuipa Real Madrid ya kocha Zinedine Zidane fursa bora zaidi ya kujivunia huduma za fowadi huyo.

Tottenham ni kikosi cha kwanza cha EPL kupunguza mshahara wa wafanyakazi 550 wasiokuwa wachezaji huku Levy akisisitiza kwamba virusi vya homa ya corona vimewaathiri sana kiuchumi hasa ikizingatiwa kwamba vinara wa klabu hiyo walitumia fedha nyingi mno kujenga uwanja wao mpya wa Tottenham Hotspur nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, huenda Tottenham wakawa radhi zaidi kumuuza Kane ili kupunguza gharama ya kumdumisha kimshahara na pia wajipe fedha zitakazowawezesha kujisuka upya.

Ukubwa wa gharama ya kuwadumisha baadhi ya masupastaa wao, ni kati ya sababu zilizowachochea Tottenham pia kuagana na kiungo matata mzawa wa Denmark, Christian Eriksen aliyejiunga na Inter Milan ya Italia mwanzoni mwa mwaka huu.

Sh28 bilioni ni kima cha pesa zilizotumiwa na miamba wa soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) kujitwalia huduma za nyota Neymar Jr kutoka Barcelona, Uhispania mnamo 2017.

Hata hivyo, upo utata mwingi kuhusu jinsi vikosi vya soka ya bara Ulaya vitakavyojishughulisha katika soka la uhamisho wa wachezaji mwishoni mwa msimu huu kutokana na athari nyingi za kifedha zinazozidi kushuhudiwa na klabu mbalimbali kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Katika juhudi za kulijaza pengo la Kane na Eriksen, Tottenham wamefichua azma ya kumsajili kiungo Geoffrey Kondogbia, 27, kwa kima cha Sh9.8 bilioni.

Hii ni baada ya nyota huyo mzawa wa Ufaransa kusisitiza kwamba atakuwa radhi kuagana na Valencia iwapo kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) hakitafanikiwa kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Hata hivyo, itawalazimu Tottenham kuwapiga kumbo Everton ambao pia wanakeshea maarifa ya Kondogbia. Hadi alipotua Valencia, sogora huyo alikuwa pia amewachezea Lens, Sevilla, AS Monaco na Inter Milan.

Iwapo Tottenham wataambulia pakavu katika juhudi za kuwania huduma za Kondogbia, kocha Jose Mourinho amedokeza uwezekano wa kuifukuzia saini ya kiungo wa Barcelona Philippe Coutinho ambaye kwa sasa anachezea Bayern Munich ya Ujerumani kwa mkopo.

Chelsea pia wanayakeshea maarifa ya Coutinho ambaye Bayern watakuwa radhi kabisa kumwachilia iwapo watafaulu kumpata Roberto Firmino wa Liverpool pamoja na kiungo wa Manchester City, Leroy Sane.

Kwa mujibu wa kocha Hansi Flick, 55, wa Bayern, Firmino ambaye ni mzawa wa Brazil atakuwa kizibo kamili cha mvamizi Robert Lewandowski, 32, atakayeagana nao mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Mbali na Tottenham na Everton, klabu nyingine inayomezea mate huduma za Kondogbia ni Manchester United ambayo inakabiliwa na mtanziko wa ama kumsajili chipukizi Jadon Sancho wa Borussia Dortmund au kumpokeza fowadi Odion Ighalo, 30, mkataba wa kudumu ugani Old Trafford.