HabariVideo

Hauwezi kumlazimishia Miguna jambo – Ombeta

May 17th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI Cliff Ombeta alithibitisha Alhamisi kuwa Gavana Mike Sonko alimteua mwanaharakati na wakili Dkt Miguna Miguna kuwa naibu gavana wake Jumatano jioni.

Bw Ombeta aliambia Taifa Leo kuwa Gavana Sonko alimwita kisha akampa idhini ya kuandika barua ya uteuzi iliyowasilishwa kwa Spika wa bunge la kaunti, Beatrice Elachi.

“Ni kweli, Bw Sonko aliandika barua hiyo,” alisema Bw Ombeta.

Alisema alimtumia mteja wake (Dkt Miguna) nakala ya barua hiyo mtandaoni akiwa nchini Canada.

“Je, unafikiri Dkt Miguna atakubali uteuzi huu ama itaonekana ni kuchezewa akili ni Bw Sonko?” alihoji mwanahabari.

“Itetegemea na Dkt Miguna mwenyewe. Wajua tena Miguna Miguna si mtu ambaye unaweza kumlazimishia jambo. Yeye mwenyewe ataamua na kuambia umma uamuzi wake. Ikiwa atakubali au kukataa, hiyo ni haki yake,” akajibu.

Mwanaharakati huyo alikuwa akiwania kiti cha Ugavana Nairobi kwa tikiti ya chama cha Orange Democratic Movement na kushindwa na Bw Sonko.

Tangu Bw Polycarp Igathe ajiuzulu Bw Sonko amekuwa akishinikizwa amteue naibu wake.

Bunge la kaunti ya Nairobi limempa siku saba kufanya hivyo.

Video Gallery