Siasa

Havi azimwa na polisi akitaka kuvuruga wabunge

October 12th, 2020 1 min read

NA CHARLES WASONGA

BW Nelson Havi ambaye ni rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Jumatatu aliongoza ujumbe wa mawakili 20 na wanaharakati wengine kuvuruga bunge lakini wakazuiwa na polisi.

Bw Havi ambaye pamoja na Naibu Gavana wa Nairobi Jonathan Mweke walioongoza msafara huo walizuiwa kwenye lango la Bunge la Kitaifa na karibu maafisa 10 kutoka kituo cha polisi cha bunge.

Bw Mweke ni mwenyekiti mwenza wa chama kipya cha kisiasa kwa jina United Green Movement (UGM).

Walitaka kudhibiti bunge na kuwazuia wabunge kuendesha shughuli zao za kawaida wakidai wabunge hawako huko kihalali kwa sababu wameshindwa kupitisha sheria ya uwakilisha sawa wa kijinsia.

Kwenye lango la bunge, Havi na wenzake walibishana na walinzi wa bunge wakitaka waruhusiwe waingie lakini wakakatazwa.

“Kama tulivyoahidi katika barua yetu wanachama wetu walioko hapa ni ishirini pekee. Ndiposa twataka turuhusiwe tuingie,” akasema Bw Havi.

Hata hivyo, walinzi wa bunge walisisitiza kuwa ni wanne pekee wangeruhusiwa kuingia; wanaume wawili na wanawake wawili.

“Usimamizi wa bunge umetoa amri kwamba muwakilishwa na watu wanne pekee. Hii ni kulingana na masharti ya Wizara ya Afya kuhusu udhibiti wa msambao wa virusi vya corona msongamano wa watu hauruhusiwi,” akasema afisa mmoja wa idara ya ulinzi bungeni.

Bw Havi amekuwa akishikilia kuwa bunge lilipasa kuvunjwa ifikapo Jumatatu, Oktoba 12, 2020, siku 21 baada ya Jaji Mkuu David Maraga kutoa ushauri kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Wiki jana LSK iliandika barua kwa polisi ikiwaarifu kuwa wanachama wake wataelekea bungeni kushinikiza kuvunjiliwa kwa bunge, kulingana na ushauri wa Bw Maraga. Nakala za barua hiyo zilitumiwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka.