HAWA LEICESTER: Bao la Youri Tielemans kwenye fainali lawapa The Foxes Kombe la FA

HAWA LEICESTER: Bao la Youri Tielemans kwenye fainali lawapa The Foxes Kombe la FA

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

BAADA ya kusubiri kwa nusu karne, hatimaye Leicester City ilibeba Kombe la FA baada ya kuikomoa Chelsea mnamo Jumamosi usiku ugani Wembley, Uingereza.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu 1969 kwa Leicester, almaarufu The Foxes, kunogesha fainali ya kipute hicho; na katika jaribio lao hilo la tano walitawazwa wafalme.

Ushindi huo ulifanya kikosi cha kocha Brendan Rodgers kuwa timu ya 44 tofauti kunyanyua Kombe la FA katika historia ya soka ya Uingereza.

Bao la pekee kwenye mchuano huo – uliohudhuriwa na takriban mashabiki 20,000 – lilifungwa na kiungo Youri Tielemans, aliyevurumisha kombora kali kutoka hatua 25 na kumwacha hoi kipa Kepa Arrizabalaga.

Tielemans sasa ndiye mchezaji wa tatu raia wa Ubelgiji kuwahi kufunga bao kwenye fainali ya FA; baada ya Eden Hazard (Chelsea, 2017-18) na Kevin de Bruyne (Man-City, 2018-19) huku kila mmoja wao akiishia kunyanyua ubingwa wa taji hilo msimu huo.

Mara ya mwisho kwa Leicester – inayojivunia ufufuo mkubwa chini ya Rodgers – kutinga fainali yoyote ya haiba ni mwaka 2,000 wakipepeta Tranmere Rovers 2-1 ugani Wembley na kutia kapuni ufalme wa League Cup.

Katika mechi ya Jumamosi, kipa Kasper Schmeichel aliwanyima Ben Chilwell na Mason Mount nafasi za wazi kufungia Chelsea.

“Siwezi kabisa kuelezea furaha yangu. Ninapofikiria kuhusu vikosi ambavyo vimewahi kutwaa Kombe la FA hapo awali, nasi sasa tunajumuishwa kwenye orodha hiyo, naona ni zaidi ya ndoto,” akasema mlinda-lango huyo raia wa Denmark.

Schmeichel ndiye kipa wa kwanza baada ya David Seaman (Arsenal, 2003) kuongoza kikosi kushinda Kombe la FA Cup akivalia utepe wa unahodha.

“Ni tija na fahari tele kuhusishwa na Leicester wakati huu. Najivunia kuwa sehemu ya historia kwa kuwa ni tukio spesheli kunyanyulia kikosi hiki Kombe la FA kwa mara ya kwanza,” akatanguliza kocha Rodgers aliye raia wa Ireland Kaskazini.

Rodgers, ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Liverpool na Celtic (Scotland), anakuwa kocha wa kwanza baada ya Sir Alex Ferguson kubeba Kombe la FA nchini Uingereza na Scotland.

Baada ya kutawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16 kwa mara ya kwanza katika miaka 132, Leicester waliambulia nafasi ya tano kwenye ligi muhula uliofuata.

Sasa wameshinda FA watafukuzia fursa ya kukamilisha kmsimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa kindumbwendumbwe cha UEFA msimu ujao.

Watakutana tena na Chelsea katika gozi la EPL hapo kesho ugani Stamford Bridge, naa ushindi utawakatia tiketi ya kunogesha UEFA kwa mara ya pili baada ya kubanduliwa hatua ya robo-fainali mnamo 2016-17.

“Tuna nafasi nyingine maridhawa ya kudhihirisha ubabe wetu. Kushinda Chelsea katika mechi ijayo ni jambo linalowezekana,” akaongeza Rodgers aliyewahi kuongoza Celtic ya Scotland kunyanyua mataji saba chini ya miaka mitatu pekee ya ukocha.

Foxes wanashikilia nafasi ya tatu kwenye jedwali la EPL kwa alama 66 na watafunga rasmi kampeni za msimu huu dhidi ya Spurs Jumapili ijayo ugani King Power.

Kichapo kutoka kwa Leicester kiliendeleza masaibu ya Chelsea, ambao chini ya kocha Thomas Tuchel sasa wana presha ya kumaliza msimu ndani ya nne-bora na pia kushinda Man-City kwenye fainali ya UEFA mnamo Mei 29 jijini Porto, Ureno.

Chelsea ndicho kikosi cha kwanza kuwahi kupoteza fainali ya FA kwa misimu miwili mfululizo; tangu Newcastle United wafanye hivyo mnamo 1997-98 na 1998-99.

Mabingwa hao wa EPL msimu 2016-17 walipigwa 2-1 na Arsenal mwaka 2020 chini ya kocha Frank Lampard, aliyepigwa kalamu mwezi Januari na nafasi yake kutwaliwa na Tuchel.

Tuchel amewahi pia kutia makali vikosi vya Borussia Dortmund (Ujerumani) na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

Mechi kati ya Chelsea na Leicester ilikuwa fainali ya 45 ya FA kukamilika 1-0 kwa zaidi ya misimu 20.

Gozi hilo lilimpa straika Olivier Giroud wa Chelsea fursa ya kusakata fainali ya FA kwa mara ya sita. Ni Ashley Cole (8), Ryan Giggs (7) na Roy Keane (7) pekee ambao wametandaza idadi kubwa zaidi ya fainali za kipute hicho.

Akiwa na umri wa miaka 37 na siku 114, beki Wes Morgan wa Leicester sasa ndiye mchezaji mkongwe zaidi kushiriki fainali ya FA baada ya Teddy Sheringham (miaka 40 na siku 41) na West Ham United mnamo 2006.

You can share this post!

Vifo 174 na mahangaiko Israeli ikizidi kuwalipua Wapalestina

Zidane atupilia mbali madai kwamba atajiengua kambini mwa...