Hawana jipya hao, Mutua awasuta viongozi wa OKA

Hawana jipya hao, Mutua awasuta viongozi wa OKA

Na SAMMY WAWERU

GAVANA wa Kaunti ya Machakos Dkt Alfred Mutua ameicharura Okoa Kenya Alliance (OKA) akiitaja kama muungano wa viongozi wenye malengo ya kutaka kujinufaisha.

Dkt Mutua amesema Alhamisi viongozi walioasisi muungano huo ni waliohudumu katika serikali za awali, na kulingana naye haoni mabadiliko watakayoleta endapo watafua dafu kuunda serikali ijayo.

“Ni walewale tu waliohudumu katika serikali za awali. Ni mabadiliko yapi wataletea wananchi kuboresha maisha yao ambayo hawakufanya wakiwa mamlakani?” Gavana Mutua akahoji.

OKA inajumuisha kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, Bw Kalonzo Musyoka (Wiper), kiongozi wa Ford-Kenya Bw Moses Wetangula na seneta wa Baringo Bw Gideon Moi (KANU).

Mabw Mudavadi na Kalonzo wameeleza azma yao kuwania kiti cha urais mwaka ujao, 2022.

Aidha, Mudavadi amewahi kuhudumu kama makamu wa rais chini ya utawala wa Rais mstaafu Daniel Arap Moi ambaye kwa sasa ni marehemu, naye Kalonzo makamu wa rais katika serikali ya Rais mstaafu Mwai Kibaki.

“Hata ingawa tuna wanasiasa bora waliowahi kuhudumu katika serikali za hapo awali, Kenya inahitaji viongozi wapya wenye maono kuiboresha,” Dkt Mutua akasema.

Kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap ni kati ya viongozi na wanasiasa waliotangaza nia yao kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Ruto afikirie upya kuhusu kubuni...

KAMAU: Vyombo vya habari vyafaa viwajibike 2022 ikikaribia