Michezo

Haya ya De Gea ni tamaa mbele mauti nyuma

May 6th, 2019 2 min read

NA JOB MOKAYA

KIPA wa Manchester United, David De Gea amejipata matatani baada ya kuacha mipira myepesi kabisa kupita na kujaajaa kimiani mwake na kusababisha mabao yaliyomfanya aonekane kama kichekesho kikubwa miongoni mwa walinda-lango.

Juma lililopita, De Gea alifanya kosa jingine lililosababisha Chelsea kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Man-United katika mtanange uliotandazwa ugani Old Trafford. Mlinda-lango huyu amejipata matatani katika siku za hivi karibuni ambapo alifanya makosa ya kijinga katika mechi muhimu kwa waajiri wake Man- United. Makosa kama haya hayatarajiwi kutoka kwake; kipa wa haiba kubwa anayeheshima duniani.

De Gea ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Uhispania alichangia pakubwa kushindwa kwa Man-United dhidi ya Barcelona majuma mawili yaliyopita. Kushindwa kwao kulichangia kubanduliwa kwa miamba hao wa soka ya Uingereza nje ya mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ambao sasa umefikia hatua ya nusu-fainali au nne-bora.

Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni. Kabla ya mchuano wa Barcelona, De Gea alishindwa kukamata mkwaju hafifu uliopigwa na Leroy Sane katika gozi kali la Manchester na kufanya Man-United kushindwa nyumbani kwao kwa kichapo cha magoli mawili kwa yai.

Na kabla ya hata mate kukauka, Chelsea walizuru Old Trafford nayo Man-United ilinuia kubadili msururu wa matokeo hafifu kwa kuishinda Chelsea. Hata hivyo, hilo halikutokea kwani De Gea alipangua mkwaju hafifu kutoka kwa Antonio Rudiger na kuupeleka alikokuwa Marcos Alonso aliyesawazisha kutoka eneo finyu.

Man-United ilikuwa imechukua uongozi wa mapema kutoka kwa Juan Mata aliyefunga dhidi ya timu yake ya zamani lakini kosa la De Gea lilisababisha Chelsea almaarufu ‘The Blues’ warejee tena mchezoni. Huenda makosa haya ya De Gea yamesababishwa na tamaa ya kujitakia makuu.

Kwa kipindi kirefu, klabu ya Real Madrid imekuwa ikisaka huduma za De Gea huku Man-United ikikataa katakata kumuuza kipa wao nambari moja.

Hata hivyo, ndoto ya De Gea kutua Uhispania ilielekea kugonga mwamba pale ambapo Real ilifaulu kumsajili Thibaut Courtois kutoka Chelsea.

Hata hivyo, huenda ndoto hiyo ikafufuliwa tena baada ya Courtois kusajili matokeo hafifu uwanjani Santiago Bernabeu. Lile linalochangia zaidi matokeo hafifu kwa De Gea ni kile kiburi kilichosheheni akilini mwake kutokana na kuwindwa na Real na hata PSG ya Ufaransa. Kiburi hicho kimemfanya atake nyongeza ya mshahara mara dufu.

Kwa sasa, De Gea anapokea kiticha cha pauni milioni 10 kwa mwaka sawa na shilingi milioni mia mbili kwa mwezi kwa sarafu ya Kenya. De Gea ametishia kuondoka Old Trafford endapo mshahara wake hautaongezwa na kufikia shilingi nusu bilioni kwa mwezi, sawa na shilingi milioni mia moja hamsini kwa mwezi.

Aidha, De Gea anataka awe mchezaji anayepeleka nyumbani donge nono zaidi ugani Old Trafford na Uingereza nzima. Kwa sasa, Alexis Sanchez ndiye anayelipwa pesa nyingi zaidi Old Trafford na katika kipute kizima cha EPL kwa kutia kapuni kitita cha shilingi nusu bilioni kwa mwezi bila kucheza mchezo wowote.

Tamaa hii basi ndiyo imeingia akilini mwa De Gea hadi akiwa langoni, aonacho tu ni pesa, ujira mnono, vimulimuli na maisha bora nje ya London. Haoni mpira. Tamaa hii itamponza.