Michezo

Hazard kuongoza taifa 'kunyonga' wanyonge

October 10th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

BRUSELSS, Ubelgiji

KIUNGO mshambuliaji Eden Hazard ataongoza kikosi cha Ubelgiji kuendeleza rekodi yao ya asilimia 100 ya kutoshindwa watakapokabiliana na San Marino ugani King Baudouin kwenye mechi ya kufuzu kwa fainali za Euro 2020.

Kwa jumla rekodi ya Ubelgiji katika mechi saba za karibuni ni kubwa zaidi ambapo vijana hao wa kocha Roberto Martinez hawakufungwa hata bao moja.

Wakicheza nyumbani, Ubelgiji wanajivunia rekodi ya kutofungwa katika mechi mechi za karibuni. Walipokutana mwezi uliopita, Ubelgiji waliibuka na ushindi wa mabao 4-0 nyumbani.

Ubelgiji inayoongoza Kundi I kwa alama 18, inachuana kwenye kundi hili pamoja na Urusi yenye alama 15, Kazakhstan, Cyprus, Scotland na San Marino.

Kikosi hiki cha Roberto Martinez pia kitawategemea miamba Divock Origi anayechezea Liverpool, Romelu Lukaku wa Inter Milan ya Italia na Dries Mertens wa Napoli pia ya Italia.

Thibaut Courtois anayechezea Real Madrid anatarajiwa kuanza mchumani huku Thomas Vermaelen na Toby Alderweireld wakitunza ngome ya majabali hao waliofika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka jana.

Nduguye Eden, Thorgan Hazard na Michy Batshuayi watakuwa mhimili mzuri katika safu ya kiungo.

Adnan Januzaj anatazamiwa kushirikiana vyema na Origi na Hazard katika safu ya ushambuliaji dhidi ya San Marino.

Kwenye mechi hizi, Uingereza inaongoza Kundi A kwa alama 12, tatu mbele ya Jamhuri ya Czech inayofuatia.

Ukraine yenye alama 13, tano mbele ya Ureno, inayofuatia inaongoza Kundi B, huku Ujerumani kwa pamoja na Ireland Kaskazini zikiongoza Kundi C kwa alama 12.

Ireland inashikilia kilele cha Kundi D kwa pointi 11, mbili mbele ya nambari mbili Denmark.

Katika Kundi E, Croatia yenye alama 10 na Slovakia yenye alama 9 zinakamata nafasi nzuri za kufuzu. Uhispania na Sweden zinakaa juu ya jedwali la Kundi F kwa alama 18 na 11 huku Poland (13) na Slovenia (11) zikiongoza Kundi G mtawalia.

Timu zilizo katika nafasi nzuri ya kufuzu katika Kundi H ni Uturuki na Ufaransa zenye alama 15 kila moja huku Italia na Finland ziking’aa katika Kundi J kwa alama 18 na 12 mtawalia.

Ratiba: Kazakhstan na Cyprus; Belarus na Estonia; Slavakia na Wales; Rusia na Scotland, Uholanzi na Ireland Kaskazini, Latvia na Poland; Ubelgiji na San Marino; Croatia na Hungary, Macedonia Kaskazini na Slovenia halafu Austria na Israel.