Habari Mseto

Hedimasta pabaya kuzuia wanafunzi kuenda darasa la 8

December 10th, 2018 1 min read

RUSHDIE OUDIA na CAROLINE MUNDU

WAZAZI katika shule moja katika Kaunti ya Siaya wametishia kumshtaki mwalimu wake mkuu na Wizara ya Elimu kwa kuwazuia wanafunzi karibu 30 wa darasa la saba kwenda katika darasa la nane.

Mwalimu huyo anadaiwa kuwazuia wanafunzi hao kwenda katika darasa la nane kwa kukosa kufikisha alama 300 kati ya 500 katika mitihani yao ya muhula wa tatu.

Kwenye barua waliyomwandikia Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti (CDE), wazazi katika Shule ya Msingi ya Siaya Central walisema kwamba kitendo hicho hakifai, kwani kimewafanya baadhi ya wanafunzi kuacha shule.

Mwalimu mkuu, aliyetambuliwa kama George Ochieng anadaiwa kuweka kanuni hizo kali ambazo zimewatamausha baadhi ya wanafunzi.

Kutokana na hayo, wazazi hao wamempa mwalimu huyo matakaa ya siku saba kuwaruhusu wanafunzi hao 32 kuendeleza masomo yao la sivyo wamshtaki. Mbali na hayo, wanamtaka kuwasajili kwa mitihani ya kitaifa.

Wanafunzi hao walijulishwa mwishoni mwa muhula huo kwamba hawataenda katika darasa la nane, hivyo warudie darasa la saba la sivyo watafute shule nyingine.

kwingineko ikiwa lazima wasajiliwe kwa Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka ujao.

Kwenye barua waliyoandika kupitia wakili wao Evans Oruenji, wazazi walieleza jinsi hatua hiyo ilivyoaathiri kiakili pamoja na wanafunzi hao.

“Ni hatia kuwanyima haki wanafunzi kuendelea na masomo yao bila sababu zozote za kimsingi. Hii ni dhuluma ya wazi kwao,” akasema Bw Oruenjo kwa niaba ya wazazi hao.

Wakili huyo alidai kwamba mwalimu mkuu huyo amekuwa na tabia ya kuwashinikiza wazazi ambao watoto hao hawafikishi alama zilizowekwa kutafuta kwingineko kwa miaka kumi aliyohudumu katika shule hiyo.

“Hii ni njia ya mkato ya kuitafutia shule matokeo mazuri ya mtihani. Tutahakikisha tumeipinga,” akasema.