Habari za Kaunti

Hepi yarejea Diani

May 29th, 2024 3 min read

NA SIAGO CECE

MBWEMBWE za tafrija usiku zimeanza kurejea Diani polepole baada ya taa za barabarani kuwekwa katika mji huo wa Kaunti ya Kwale.

Kwa zaidi ya miaka mitano, wakazi na watalii wamekuwa wakiendesha shughuli zao kwa hofu usiku kwa sababu ya changamoto za kiusalama. Hali hii ilisababishwa na kukosekana kwa taa za barabarani kwenye barabara maarufu ya Diani Beach.

Taa za barabarani zinazotumia miale ya jua ambazo zilikuwa zimewekwa mwaka wa 2013, ziliharibiwa wezi walipoiba sola, chaja za sola na balbu na kuacha mitaa kwa giza tupu usiku.

Hali hii ilifanya watalii kutembea usiku kurudi kwa vyumba vyao wakitoka maeneo ya burudani.

Barabara ya Twj pia inatumika kufikia hoteli za ufuoni na hoteli zenye vyakula na huduma za kiasili.

Diani, ambao ni mji wa mapumziko, umekuwa ukiwavutia watalii kutoka duniani kote duniani na maeneo mengine ya ukanda wa Pwani ya Kenya kama vile Mombasa na Kilifi. Wageni hao hutumbuizwa katika vilabu maarufu vilivyoko katika eneo hilo.

Baadhi ya vilabu vyenye umaarufu mkubwa ni Full Moon Club, Manyatta Disco, Palmer Club, na Tandoori International Club na vyote hivi viko pembezoni mwa barabara ya Beach.

Mradi wa serikali ya kaunti kutundika upya taa katika barabara hiyo kumeamsha tena eneo hilo, ambapo watalii na wapenda tafrija hufurika usiku kujipa raha.

Kaunti nayo inatarajia kujiongezea mapato yake kutokana na utalii.

Kulingana na Gavana wa Kwale Fatuma Achani, hatua hiyo ilikuwa ya kusaidia kupiga jeki na kujenga mazingira ya watu kufanya kazi saa 24 kukuza biashara ndogondogo na za kadri.

Kabla ya mradi huo wa uboreshaji, hali ilikuwa mbaya sana hivi kwamba wakazi walikuwa wakiondoka barabarani mara giza lilipoingia. Hii iliathiri biashara zinazowalenga wateja wa nyakati za usiku.

Mara si moja, watalii walikuwa wakivamiwa na wezi, huku wakinyang’anywa simu zao katika barabara za mji wa diwani.

Lakini sasa ukaguzi wa Taifa Leo umegundua kwamba shughuli za usiku zimeongezeka tena kwenye barabara ya Beach baada ya taa mpya za barabarani kuwekwa.

“Zamani tulikuwa tunapokea visa vingi vya watu kuibiwa mali zao barabarani. Katika mazingira ya giza vichochoro, magenge yalikuwa yakitegea watalii na kuwashambulia usiku,” akasema Kamanda wa Polisi wa Msambweni Bw Francis Gachoki

Aliongeza kwamba tangu taa kuwekwa, kesi za aina hiyo zimerudi chini mno.

“Tunashukuru Serikali ya Kaunti kwa sababu watalii wengi sasa wanaweza kutembea barabarani bila uoga,” alisema kwenye mahojiano.

Aliongeza kuwa taa hizo pia zinasaidia polisi kushika doria na kudadarukia changamoto za kiusalama wanapopata taarifa kuhusu uwepo wa magenge ya uhalifu katika eneo fulani.

Wadau wa sekta za utalii na burudani wamepongeza kuwekwa kwa taa hizo tangu Machi 2024, wakisema mwangaza na usalama wa kutosha utasaidia biashara zao kuimarika zaidi.

Bw Stephen Mure, ambaye ni meneja wa burudani katika kampuni ya kutoa burudani ya Sisi Kwa Sisi Entertainment Movement, alisema kwa sasa wanaweza kuandaa tafrija za usiku ambazo zitavutia watu wengi zaidi.

Alisema mara kwa mara, sherehe za tafrija katika siku za wiki na wikendi vilevile, huandaliwa ambapo wasanii maarufu na watumbuizaji (madijei) huzinogesha.

“Idadi ya watu waliokuwa wakijitolea kupiga sherehe ilikuwa imepungua kwa sababu ya ukosefu wa usalama wa kutosha. Watu wengi hawakupendelea kupata burudani hadi chee, walikuwa wakipendelea kuondoka mapema kabla saa sita usiku,” akasema Bw Mure.

Alisema ingawa huu ni msimu wa idadi ndogo ya watalii, biashara inatarajiwa kuamka mwishoni mwa Julai wakati wa msimu wa kilele cha utalii utaanza.

Alitoa wito kwa kaunti kuhakikisha barabara za kuelekea katika hoteli za Jacaranda Beach na Neptune Beach nazo pia zinawekwa taa.

Waziri wa Biashara na Utalii wa Kwale Michael Mutua, alisema lengo la kuweka taa ni kuhakikisha utalii unakua katika kaunti hiyo.

“Watalii hupendelea kutembea barabarani usiku baada ya mlo na vinywaji. Ndio maana wengi wanapendelea Diani kwa sababu ya hepi inayokoleza raha usiku,” akasema Bw Mutua.

Aliongeza kwamba baada ya taa za sola kung’olewa, kaunti ililazimika kutumia teknolojia ya kisasa kuhakikisha taa mpya haziibiwi.