Makala

‘Hesabu ya Cherera’ yazuka chuo kikuu cha Dedan Kimathi kugawa Sh180 za Rais Ruto

April 14th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

VITA vya kimaneno vimezuka kati ya wasimamizi wa chuo kikuu cha Dedan Kimathi (DeKUT) na muungano wa wanafunzi (DeKUTSO) kuhusu zawadi ya Sh1 milioni ambayo Rais William Ruto aliwazawadi hivi majuzi.

Rais Ruto alikuwa ametembea chuo hicho kwa ziara ya kikazi Machi 26, 2024 na kama zawadi yake ya kibinafsi kwa wanafunzi hao, akawapa mchango huo wajivinjari nao.

Katika hali ya wasimamizi wa chuo hicho kusaka mbinu ya kutumia kitita hicho, mshirikishi wa masuala ya wanafunzi Dkt Esther Nthiga alitoa taarifa Aprili 9, 2024 akisema kwamba alitekeleza kura ya maoni ambayo ilitoa matokeo kwamba wanafunzi hao walipendelea kugawana pesa hiyo.

Katika kura hiyo, Dkt Nthiga alisema kwamba asilimia 51 ilipendelea pesa hizo zigawanwe na wanafunzi ambapo kila mmoja angepata Sh180.

Asilimia 36.4 ilipiga kura ya pesa hizo ziwekwe kwa hazina ya basari huku nayo asilimia 35.5 ikipendelea kuandaliwe mlo wa pamoja.

Kura hiyo iliashiria kwamba wanafunzi 5, 556 ndio wangenufaika na pesa hizo.

Hata hivyo, ukijumuisha asilimia za waliopiga kura hiyo, utapata kwamba kura hiyo ilishirikisha asilimia 122.9 ya wanafunzi badala ya asilimia 100 hivyo basi kuzua swali la ni wapi maoni ya ziada kwa kiwango cha asilimia 22.9 yalitoka.

Hesabu hiyo imesutwa kuwa sawa na iliyotolewa na aliyekuwa Kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhusu kura ya urais ya 2022 ambapo alidai matokeo yalikuwa yamezidi wapiga kura kwa asilimia 0.01(100.01) badala ya 100.

Baada ya chuo hicho kutoa taarifa hiyo iliyowaelekeza wanafunzi waanze kufika katika afisi ya hazina kuchukua mgao wa Sh180, muungano wa wanafunzi kupitia katibu mkuu Bw Nicholas Ng’etich umeteta kwamba haukuhusishwa.

“Hakuna uwiano kati ya wanafunzi na chuo cha Dedan Kimathi kuhusu zawadi ya Rais. Taarifa ya Dkt Nthiga haina maafikiano na muungano wa wanafunzi na tunaichukulia kama njama ya kutuhujumu kama wasimamizi wa wanafunzi wa DeKUT,” akasema.

Hata hivyo, Bw Ng’etich hakutoa mwelekeo faafu kwa wanafunzi kwa mujibu wa muungano huo kuhusu jinsi ya kutumia kitita hicho cha Rais Ruto.

[email protected]