Hesabu yakanganya makamishna walioasi matokeo ya urais

Hesabu yakanganya makamishna walioasi matokeo ya urais

NA BENSON MATHEKA

MAKAMISHNA wanne ambao wamejitenga na matokeo yaliyotumika kumtangaza Naibu Rais William Ruto kuwa mshindi wa urais kwenye uchaguzi wa Agosti 9, wamejikanganya kwenye ufafanuzi wao kuhusu sababu ya kumuasi mwenyekiti wao Wafula Chebukati.

Kwenye kikao na wanahabari katika hoteli ya Serena muda mfupi kabla ya mwaniaji wa Azimio Raila Odinga kutoa taarifa yake katika jumba la KICC, makamishna hao walipotosha waliposema kuwa idadi ya kura ambazo zilipita asilimia 100 ni 142,000.Hii ni kufuatia takwimu zilizoonyesha kuwa asilimia waliyozoa wawaniaji urais ilikuwa asilimia 100.01 badala ya asilimia 100.

“Takwimu za Bw Chebukati ni za kuaibisha. Ukiongeza asilimia ya kila mwaniaji utapata asilimia 0.01 zaidi ya asilimia 100. Hii ni sawa na kura 142,000 ya jumla ya zilizopigwa. Swali ni kuwa hizi kura zilitoka wapi na zilipewa nani?,” akasema Naibu Mwenyekiti wa IEBC, Julian Cherera.

Lakini ukweli ni kuwa, asilimia 0.01 ya kura 14,213,137 za wagombeaji wote ni 1,421 pekee. Makamishna hao walikuwa wametoa hiyo kama sababu yao kujitenga na matokeo ambayo Bw Chebukati alitangaza mnamo Jumanne yakionyesha Dkt Ruto kuwa rais mteule kwa kuzoa jumla ya kura 7,176,141, mbele ya Bw Odinga aliyepata 6,942,930.

Sababu nyingine ambayo Bi Cherera na makamishna wenzake Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi walitoa ni kuwa, Bw Chebukati alikataa kuwaonyesha jinsi alivyoweza kufikia matokeo ambayo alitangaza.

“Tulitaka kupata nakala ya matokeo ndiposa tuyakague na kutathmini kabla hayajatangazwa lakini Bw Chebukati akakataa. Hii ni moja ya sababu iliyofanya tujitenge na matokeo aliyotangaza,” akaeleza Bi Cherera.

Makamishna hao wanne walidai Bw Chebukati alitangaza matokeo kabla ya mchakato wa kuyajumlisha kukamilika na kwamba, hakuwaruhusu kuthibitisha na kuidhinisha matokeo hayo kabla ya kutangazwa.

“Tulifikia uamuzi kwamba, mchakato uliotumiwa kuandaa Fomu 34C kumtangaza Dkt Ruto haukuwa wa wazi. Wakati ambao Wafula Chebukati alitangaza matokeo, uthibitishaji wa matokeo kutoka baadhi ya maeneo bunge haukuwa umetangazwa,” alisema Bi Cherera.

Makamishna hao walisema waliamua kuondoka Bomas Of Kenya kabla ya Bw Chebukati kutangaza matokeo kwa sababu hawakutaka kuwa sehemu ya matokeo ambayo hawakuthibitisha.

“Ndiposa tunasisitiza kuwa hatutambui matokeo yaliyotangazwa na Bw Chebukati,” akasisitiza.

Hata hivyo, walisema kwamba ni jukumu la Bw Chebukati kutangaza matokeo ya urais.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Viongozi wanawake waungwe mkono ili wafaulu...

Kenya Kwanza kufanya mkutano wa kwanza

T L