Hichilema aapishwa huku raia wakitarajia mwamko mpya

Hichilema aapishwa huku raia wakitarajia mwamko mpya

Na AFP

LUSAKA, ZAMBIA

HAKAINDE Hichilema, 59, sasa ndiye rais mpya wa Zambia baada ya kuapishwa Jumanne katika hafla iliyohudhuriwa na marais wa sasa na waliotangulia, wajumbe na viongozi wa upinzani kutoka mataifa ya Bara la Afrika.

Kiongozi huyo wa upinzani alimbwaga rais aliyekuwa afisini, Edgar Lungu, 64, katika jaribio lake la sita la kuwania urais, kwenye uchaguzi uliofanyika Agosti 17.

Alinyakua ushindi mkubwa huku akimtangulia Lungu kwa kura karibu milioni moja katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali na uliotajwa kama hatua kuu katika demokrasia Afrika.

Matatizo ya kiuchumi na sheria kali zilizozima uhuru wa kujieleza katika utawala wa awali, zilichangia mno kumpokeza urais Hichilema na kumfanya kuwa kiongozi wa 17 kutoka kambi ya upinzani kushinda uchaguzi nchini humo.

Aliibuka mshindi licha ya kuzuiwa kufanya kampeni kikamilifu na madai ya wizi wa kura kutoka kwa chama cha Lungu, ambapo karibu asilimia 71 ya wapigakura walijitokeza huku raia wakipiga foleni hadi usiku ili tu kupiga kura.

“Lilikua jambo ambalo halikutarajiwa kuhusu azma ya watu,” Ringisai Chikohomero, mtaalam wa utafiti kutoka Kituo cha Mafunzo kuhusu Usalama, Jijini Pretoria, alielezea AFP.

Lungu na mshindani wake waliachana kwa karibu katika chaguzi za 2016 na 2015.

Umaarufu wa rais huyo anayeondoka hata hivyo ulizoroteshwa kutokana na miundomsingi duni hali iliyotumbukiza taifa hilo la Afrika Kusini lenye watu zaidi ya 18 milioni, katika madeni.

Sarafu ya nchi hiyo, kwacha, ilishuka thamani huku mfumko wa bei ukipanda kwa asilimia 24, na kufanya bei ya bidhaa kuwa ghali kupindukia katika taifa hilo ambapo zaidi ya nusu ya raia wake walikuwa wakiishi katika ufukara kabla ya janga.

Hichilema, anayefahamika vilevile kama “HH” au “Bally” – jina linalomaanisha baba – ameapa kulainisha mambo na kuvutia tena wawekezaji waliokata tamaa.

“Viongozi wa kiimla huenda wakajifunza mambo kadhaa kutokana na hili,” Mtaalam wa masuala ya kiuchumi Zambia, Grieve Chelwa alisema.

Hata hivyo, ameonya kwamba matukio ya Zambia huenda vile vile yakawa na “athari mbaya” ya kuwahimiza “madikteta” wa Kiafrika “kuzidisha wizi katika uchaguzi.”

Wachanganuzi na waangalizi wanaafikiana kwamba Lungu aliingilia shughuli ya uchaguzi, wakitaja hila za kuwatia uwoga na idadi kubwa ya wapigakura waliosajiliwa katika ngome za upinzani.

“Ulikuwa uchaguzi duni ulioingiliwa kwa njia kadhaa. Matokeo yangeweza kuvurugwa kirahisi kupendelea chama tawala ikiwa washiriki hawangekuwa wameachwa kwa mbali,” alisema mtaalam wa siasa, Nic Cheeseman. 

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Kiswahili kitukuzwe kwa vitendo badala ya...

Mamilioni yapotelea kwenye miradi duni