Makala

Hii ndio siri ya kufaulu katika biashara

March 30th, 2024 2 min read

NA BENSON MATHEKA

KABLA ya kuanzisha mradi wowote wa kibiashara, fanya utafiti kwanza, kisha utie bidii, uwaelewe wateja wako vyema na kisha uwe tayari kuvumilia changamoto zitakazoibuka.

Biashara pia inahitaji uwekezaji mzuri na inaweza kuchukua muda kabla ya kuanza kuleta faida ya haja, wanaeleza wataalamu wa biashara.

Kinachoweza kufanya mtu kutofaulu katika biashara ni kutokuwa na bidii, kuvunjika moyo na kutokuwa mwaminifu kwa wateja wake, wanasema.

“Miradi yote ya biashara inahitaji uvumilivu na uaminifu. Ikiwa mtu anavunjika moyo na kukosa kuwa mwaminifu kwa wateja wake basi hawezi kufaulu katika biashara,” aeleza Bw Joseph Suuva, mshauri wa masuala ya biashara.

Bw Suuva asema kwamba mtu anafaa kuwa na malengo fulani anapoanzisha mradi wowote wa biashara na awe anaielewa vyema. “Makosa wanaofanya Watu ni kuanzisha miradi kwa sababu watu wengine wamefanya hivyo. Hii ndio sababu yao kukosa kufaulu,” asema.

Mshauri huyu anaongeza kwamba njia nzuri ya kufaulu katika mradi wowote wa kibiashara ni kuelewa changamoto zake na kufanya utafiti wa bidhaa mpya zinazoibuka kila wakati.

“Elewa changamoto za biashara yako kisha ufanye utafiti. Tumia tekinolojia kujifunza mbinu mpya na bidhaa mpya, kufikia wateja na kutafuta soko mpya. Ukifanya hivi, hautajuta biashara yako itakuwa katika Hali nzuri ya kufaulu na hautajuta kamwe,” asema.

Wataalamu wanaonya kwamba tamaa katika biashara inaweza kutumbukiza mtu kwenye hasara kubwa.

“Fanya kila kitu kwa hatua, usiwe na tamaa. Tamaa ni mbaya na inaweza kukusababishia hasara kubwa na hata kukutia pabaya,” asema mtaalamu huyu.

Mtu akiongozwa na tamaa anaweza kuwauzia wateja bidhaa duni, hatari kwa afya na hata kuwatapeli wateja wake. Mtu wa tamaa, aeleza, anaweza pia kutumia pesa vibaya badala na kusambaratisha biashara.

Kulingana naye, wanaoanza biashara kwa mtaji wa chini huwa wanafaulu kuliko wanaowekeza pesa nyingi.

“Usiogope kuanza biashara na mtaji mdogo kwa sababu wanaofanya hivyo hufaulu. Hii ni kwa sababu wanavumilia pandashuka za biashara, wanaikuza na inajijenga na kustawi tofauti na wanaoongozwa na tamaa na kuwekeza mamilioni katika biashara,” aeleza.

Ni muhimu kuweka rekodi ya biashara yako ili ujue iwapo inafanya vyema au la. Bila rekodi, mtu hawezi kujua iwapo biashara inampa faida au la.

Anashauri watu kuwasiliana na wataalamu walioidhinishwa na serikali kwa ushauri wa kibiashara.

“Kuna wataalamu na washauri bandia na ukiwategemea biashara yako itaporomoka na upate hasara. Hivyo basi, pata huduma za wataalamu na washauri wa kiuhakika wakiwemo wanaoelewa masuala ya sheria , ushuru na usimamizi wa wafanyakazi. Haya ni mambo muhimu katika biashara yoyote,” asema.