Habari Mseto

Hii ndiyo sababu tumepiga marufuku mifuko ya sasa – NEMA

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Sababu za kupiga marufuku mikoba ya sasa ya kubeba bidhaa ni kutokana na kuwa watengenezaji wake walikataa kufuata kanuni.

Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA) imesema kuwa watengenezaji hao wanatengeneza mikoba ya ubora wa chini na ambayo haiwezi kutumiwa tena.

NEMA ilichukua hatua hiyo zaidi ya mwaka mmoja baada ya kupiga marufuku matumizi ya mikoba ya plastiki nchini.

Mamlaka hiyo ilisema haitatoa muda zaidi kwa wauzaji kumaliza mikoba hiyo kwa stoo zao baada ya muda wa mwisho, Machi 31, 2019.

Kulingana na NEMA mikoba inayotengenezwa sasa ni myembamba sana na haiwezi kutumiwa mara nyingine.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMA Geoffrey Wahungu alisema marufuku hiyo itaendelea kuwepo mpaka Mamlaka ya Kusimamia Ubora wa Bidhaa (KEBS) iweze kutambulisha uwezo na ubora wa mifuko hiyo.

Kulingana naye, watengenezaji waliharibu ubora wake ingawa walipoanza kuisambaza mara ya kwanza ilikuwa ya ubora wa juu, lakini sasa inaweza kutumiwa mara moja tu, kama mikoba ya plastiki ya awali.

NEMA ilipiga marufuku mikoba hiyo kwa kuchafua mazingira na hatua ya sasa inatarajiwa kuongeza gharama kwa watengenezaji na wanunuzi na baadaye watumiaji.

Agizo ya kukoma kutengeneza, kuuza na kutumia mikoba hiyo lilitolewa Novemba mwaka jana ila wauzaji na watengenezaji wakaomba kupewa muda zaidi.

Waliongezewa miezi mitatu mnamo Desemba baada ya mkutano na NEMA.