HabariSiasa

Hii 'reggae' ya BBI nitaizima, aapa Ezekiel Mutua

February 24th, 2020 2 min read

NA CECIL ODONGO

AFISA Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini (KFCB) Dkt Ezekiel Mutua ameonya MaDJ ambao hukodishwa kutumbuiza kwenye mikutano ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) kwamba watakamatwa kwa kucheza muziki uliopigwa marufuku.

Dkt Mutua alisema muziki ambao umekuwa ukisakatwa kwenye mikutano hiyo si wa kimaadili huku pia akiwakashifu viongozi wa kisiasa kwa kutoa matamshi yaliyosheheni lugha chafu dhidi ya wapinzani.

“Nitasimamisha ‘Reggae’ kwa kuwanyaka MaDJ wanaocheza muziki kwenye mikutano ya BBI. Wakati wa mkutano wa wikendi mjini Narok, walichezesha nyimbo ambazo nilizipiga marufuku na tutawachukulia hatua za kisheria iwapo watadhubutu kurudia hilo,” akasema Dkt Mutua Jumatatu afisini mwake.

Baadhi ya nyimbo alizolalamika zimekuwa zikichezwa mara kwa mara kwenye hafla za BBI ni ‘Tetema’ ya msanii Diamond Platnumz kutoka nchi jirani ya Tanzania na ule wa ‘Wamlambez’ ulioimbwa na kundi wanamuziki kwa jina Ethic.

Alifichua kwamba kuna muziki ambao umeteuliwa kimakusudi kutumika wakati wa mikutano ya umma na sherehe za kitaifa badala ya muziki chafu unaoyeyusha maadili na usiomtukuza Mungu.

Dkt Mutua alisema hayo wakati wa kuzindua mabalozi wa KFCB watakaohakikisha kwamba muziki na video chafu zinakomezwa katika kaunti zote 47 nchini.

Mabalozi hao watasimamiwa na mchekeshaji nguli Walter Mong’are na mwanafasheni maarufu Betty Adera.

Aidha afisa huyo alipendekeza sheria zibadilishwe ili KFCB iondoe kizuizi cha kudhibiti muziki unaochezwa kutoka saa tano asubuhi hadi saa nne usiku pekee.

“Sheria zinafaa kubadilishwa ili muda tuliowekwa wa kuhakikisha kwamba muziki na video chafu hazienei unaondolewa na KFCB kuruhusiwa kufanya kazi kwa saa 24.

“Kuna baadhi ya vipindi vichafu kwenye runinga zetu lakini huanza baada ya saa nne usiku. Ni jukumu la wazazi kuhakikisha watoto wao hawatazami vipindi hivyo,” akaongeza Dkt Mutua.

Hata hivyo, aliwasifu wahudumu wa matatu kwa kutii sheria na kukoma kuonyesha kanda za video za ngono kwenye magari yao. Pia aliwataka raia kupiga simu kupitia nambari maalum inayopatikana kwenye mtandao wao ili kuripoti magari yanayokiuka masharti ya KFCB.

Vilevile Dkt Mutua alipuuza dhana miongoni mwa Wakenya kwamba muziki au video chafu huuza na kumpa mwanamuziki umaarufu kuliko ule uliotungwa bila masuala ya ngono.

Alisema ushawishi huo hupotea baada ya muda mfupi na nyimbo hizo kusahaulika haraka.