Hii ya Ronaldo kuenda Chelsea ni hatari!

Hii ya Ronaldo kuenda Chelsea ni hatari!

Na MASHIRIKA

HUENDA Cristiano Ronaldo akabanduka ugani Old Trafford muhula huu na kuyoyomea Stamford Bridge kuvalia jezi za Chelsea wanaotiwa makali na kocha Thomas Tuchel.

Kwa mujibu wa gazeti la The Athletic, mmiliki mpya wa Chelsea, Todd Boehly, alikutana na Jorge Mendes ambaye ni wakala wa Ronaldo nchini Ureno mnamo Juni 24, 2022. Mustakabali wa Ronaldo kambini mwa Manchester United na uwezekano wake wa kuhamia Chelsea ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na wawili hao.

Licha ya Ronaldo kufungia waajiri wake mabao 24 kutokana na mechi 38 katika mashindano yote ya msimu wa 2021-22, Man-United walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) nje ya mduara wa nne-bora na hivyo kutofuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Mabingwa hao mara 20 wa EPL waliambulia nafasi ya sita na kujikatia tiketi ya kushiriki Europa League muhula ujao wa 2022-23.

Ronaldo, 37, angali na miezi 12 katika mkataba wa miaka miwili aliotia saini mnamo Agosti 2021 alipojiunga upya na Man-United baada ya kuagana na Juventus ya Italia.

Chelsea wanaohemea pia maarifa ya Raheem Sterling kutoka Manchester City, wanasaka mshambuliaji mzoefu atakayejaza pengo la Romelu Lukaku anayewaniwa upya na Inter Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

“Kufikia sasa, haijulikani iwapo Mendes na Boehly waliafikiana kuhusu uhamisho wa Ronaldo. Hilo litasalia kuwa suala la kusubiriwa. Hata hivyo, tutarajie baadhi ya mambo kufichuka chini ya siku chache zijazo,” likasema gazeti la The Mirror Sport nchini Uingereza.

Mbali na Chelsea, vikosi vingine vinavyomezea mate huduma za Ronaldo aliyebanduka Real Madrid mnamo Julai 2018 ni Bayern Munich (Ujerumani), AS Roma (Italia) na Sporting (Ureno).

Ronaldo alichezea Sporting mara 25 katika Ligi Kuu ya Ureno kabla ya kuhamia Man-United mnamo 2003. Yamekuwa matamanio makubwa ya mama wa Ronaldo, Dolores, kushuhudia mwanawe akirejea Lisbon kusakatia Sporting.

Man-United wanaonolewa sasa na kocha raia wa Uholanzi, Erik ten Hag, wana kiu ya kumdumisha Ronaldo ambaye katika mahojiano ya hivi majuzi na wanahabari alisema, “anafurahia maisha ugani Old Trafford.”

“Ten Hag alifanya kazi nzuri kambini mwa Ajax. Ni kocha mzoefu mwenye tajriba pevu. Hata hivyo, itakuwa vyema kwa Man-United kumpa muda wa kutosha ili wachezaji wazoee mbinu zake za ukufunzi. Anastahili kupewa jukwaa mwafaka la kubadilisha mambo jinsi anavyotaka,” akaeleza Ronaldo.

  • Tags

You can share this post!

Rovanpera mfalme mpya Safari Rally, Toyota iking’aa

Liverpool na Salah wavutania mshahara

T L