Habari za Kitaifa

Hiki hapa kiini cha shilingi ya Kenya kuimarika dhidi ya sarafu za kigeni


THAMANI ya shilingi ya Kenya iliimarika dhidi ya dola ya Amerika ikibadilishwa kwa Sh128, hali inayotokana na mapato kutoka kwa sekta ya utalii na kilimo.

Benki za biashara zilibadilisha shilingi 128.00/129.00 kwa dola, ikiashiria kuimarika kwa thamani kutoka 129.50/130.50 kwa dola.

Kulingana na wataalamu, kulikuwa na mahitaji makubwa ya shilingi ya Kenya huku watalii wanaozuru Kenya wakitaka kubadilisha dola zao kwa shilingi za Kenya.

Ongezeko hili la mahitaji lilichangia uhaba wa shilingi, ambao uliimarisha thamani yake katika ubadilishaji.

Ni kutokana na uthabiti wa shilingi ya Kenya, ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Kawi na Petroli (EPRA) ilitangaza kupunguza bei za mafuta kwa mwezi Juni hadi Julai.

Dizeli ilipungua kwa Ksh6.08 kwa lita, petroli aina ya Super kwa Sh3 na mafuta ya taa yakapungua kwa Sh5.71 kwa lita, na hivyo kusisitiza athari za nguvu za shilingi katika uthabiti wa bei ya mafuta.

Kutokana na hali hiyo, mafuta jijini Nairobi yanauzwa kwa Sh189.84 kwa lita ya petroli aina ya Super, Sh173.10 kwa lita kwa dizeli, na Sh163.05 kwa lita ya mafuta ya taa.

“Kuna usambazaji wa dola zaidi kuliko mahitaji. Tuna sekta ya kilimo, pia tuna sekta ya utalii,” alisema Dkt William Kemei, mtaalamu wa benki.

Wachanganuzi wa Reuters

Wachanganuzi wa Reuters nao walikadiria shilingi ya Kenya itaimarika dhidi ya dola katika muda wa wiki ijayo hadi Alhamisi kutokana na kuongezeka kwa uingiaji wa fedha za kigeni.

Vilevile, shilingi imeendelea kuimarika kufuatia kuongezeka kwa mapato ya dola kutoka sekta ya kilimo hasa kutokana na mauzo ya nje ya chai na kahawa.

Mapema wiki jana, kulikuwa na faida ambayo ilitokana na mauzo ya nje kutoka mazao ya kilimo cha bustani, chai na kahawa.

Wauzaji nje walipata kiasi kikubwa cha dola kutokana na mauzo ya mazao hayo. Wataalamu wanasema hii ilisababisha hitaji la shilingi huku wauzaji bidhaa nje wakibadilisha mapato yao ya dola kwa sarafu ya Kenya.

Shilingi imeimarika dhidi ya dola kwa muda wa miezi mitano iliyopita, hatua ambayo ilitokana na hatua kali za sera za fedha za serikali.

Katika ripoti yake ya uchanganuzi wa kiuchumi wa Aprili 2024, Benki ya Dunia iliorodhesha Shilingi ya Kenya kama sarafu inayofanya vizuri zaidi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Zaidi ya hayo, Benki Kuu ya Kenya katika Mkutano wake wa hivi majuzi wa Sera ya Fedha (MPC) ilifichua kuwa sarafu thamani ya shilingi iliongezeka kwa asilimia 17 dhidi ya sarafu nyingine za kimataifa.