Hila ya Ruto kumtetea Kalonzo

Hila ya Ruto kumtetea Kalonzo

NA BENSON MATHEKA

NAIBU RAIS William Ruto amezua mdahalo kwa kumtetea kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuteuliwa mwaniaji mwenza wa mpinzani wake mkuu Raila Odinga katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Jana Jumatano, Dkt Ruto aliungana na washirika wake kukosoa hatua Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kumtaka Bw Musyoka kufika mbele ya jopo walilounda kuteua mwaniaji mwenza wa waziri mkuu huyo wa zamani.

Jopo hilo linalojumuisha Askofu Peter Njenga, Askofu Mkuu Zacchaues Okoth, Seneta wa Kitui Enock Wambua, Michael Orwa, Dkt Noah Wekesa, Sheikh Mohammed Khalifa na Bi Beatrice Askul Moe lilipatia vyama tanzu vya Azimio hadi leo Alhamisi kuwasilisha majina ya wanaotaka kuhojiwa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

Kwenye taarifa kupitia anwani zake za mitandao ya kijamii, Dkt Ruto alisikitika kwamba kiongozi wa hadhi ya Bw Musyoka anaweza kuhojiwa na jopo hilo licha ya kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017.

“Ingawa ni wapinzani wetu, kumdhalilisha Mheshimiwa Kalonzo kwa kumshirikisha kwenye mahojiano sio haki. Ni lazima tuungane kuangamiza tabia ya udaganyifu wa kisiasa, ambao ni sifa kuu ya baadhi ya wanasiasa,” akasema Dkt Ruto.

“Hata kama hali ni gani, kila kiongozi anahitaji kuheshimiwa. Heshima si utumwa,” aliongeza Dkt Ruto.

Katika kile kilichoonekana kuwa kampeni iliyopangwa kuzua mdahalo kuhusu hatua ya Azimio ya kumtaka Bw Musyoka kuhojiwa, washirika wa Dkt Ruto waliunga kauli yake wakisema kiongozi huyo wa Wiper anafaa kuteuliwa moja kwa moja.

“Mheshimiwa Dkt Kalonzo Musyoka, Wakili Mkuu, Waziri wa Elimu, Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Makamu Rais 2008- 2013, Mgombea mwenza 2013 na 2017. Baba Raila Odinga, uko na mwaniaji mwenza. Usihojiwe na jopo. Kimbia!” Wakili Nelson Havi alimshauri Bw Musyoka.

Hata hivyo, washirika wa Bw Odinga na wachanganuzi wa siasa walisema kauli ya Dkt Ruto sio hasa ya kumtetea Bw Musyoka bali ni mbinu ya kuchochea uhasama katika kambi ya wapinzani wake.

Walishangaa jinsi Dkt Ruto anavyoweza kupinga kuhojiwa kwa Bw Musyoka ilhali yeye na hadhi yake ya unaibu rais, alihojiwa na chama chake cha United Democratic Alliance kabla ya kuteuliwa mwaniaji urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Je, William anasema alidhalilishwa alipofika mbele ya Johnson Muthama (mwenyekiti wa UDA) na Veronica Maina (Katibu wa UDA) kuhojiwa kabla ya kukabidhiwa tikiti ya kuwania urais ilhali hicho ni chama anachomiliki. Na kuhojiwa kwake kulikuwa dhuluma pia?” alihoji mchanganuzi wa siasa Tambara Geoffrey.

Mnamo Machi 2022, Dkt Ruto alifika mbele ya Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya UDA kuhojiwa kabla ya kuteuliwa rasmi kuwa mwaniaji urais wa chama hicho.

Bodi hiyo ilikataa maombi ya wawaniaji wengine wawili waliokuwa wakimezea mate tikiti ya chama hicho kugombea urais.

Bw Tambara anasema kuwa lengo la Dkt Ruto kuingilia maswala ya Azimio la Umoja One Kenya ni kutaka kuvuruga muungano huo ili ukose kura zaidi ya 1.5 milioni za ngome za Bw Musyoka.

“Hasa anacholenga ni kuvuruga kura za Ukambani ambazo anajua zitamwendea Bw Odinga, makamu rais huyo wa zamani akiwa mwaniaji mwenza wake ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa 2013 na ule wa 2017,” anasema Bw Tambara.

Bw Musyoka amenukuliwa akisema kwamba hatafika mbele ya jopo hilo kuhojiwa akisema kulingana na hadhi yake atakuwa amejidhalilisha.

Mchanganuzi wa siasa Thomas Maosa anasema kwamba ni kinaya kwa Dkt Ruto kuingilia suala la mwaniaji mwenza wa Bw Odinga ilhali hajatangaza wake.

“Huenda Dkt Ruto anataka Bw Musyoka ateuliwe ili amfungie kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua ambaye anapigiwa upatu kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga. Kuna uwezekano Dkt Ruto anataka kuteua mwanamke kutoka Mlima Kenya kuwa mwaniaji mwenza wake na Martha anaweza kuvuruga mipango yake,” asema.

Maosa anasema kila kauli ya Dkt Ruto huwa inanuiwa kutimiza maslahi ya kisiasa.

You can share this post!

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Senior...

Aliyefungwa jela maisha apata afueni ya ‘utoto’

T L