Habari

Hili tamko la Rais kuhusu maji likizingatiwa wakazi Nairobi watafurahia

August 12th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta amesema hakuna anayepaswa kuuza maji yanayosambazwa kupitia miradi ya serikali.

Kiongozi huyo wa taifa Jumatano amesema maji katika kila mtaa Kaunti ya Nairobi ni bure, kwa kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kila mwananchi anapata raslimali hiyo muhimu.

“Maji katika kila mtaa Nairobi ni ya bure. Utapeli wa wahuni kuuzia watu maji bei ghali kuliko mafuta lazima ufikie kikomo,” akaonya Rais Kenyatta, wakati akizungumza katika hafla iliyoandaliwa ukumbi wa KICC kujadili utoaji wa huduma Nairobi.

Mnamo Machi 18, 2020, Rais Kenyatta alibuni Shirika la Ustawishaji jiji la Nairobi, ndilo NMS na linaloongozwa na Meja Jenerali Mohammed Abdallah Badi.

Rais amesema tangu kubuniwa kwa NMS, zaidi ya visima 200 Nairobi vimechimbwa.

“Kila mtaa Nairobi sasa una maji safi kupitia jitihada za NMS,” akasema, akiendelea kuonya viongozi wakuu katika serikali ya Jubilee wanaojihusisha na siasa badala ya kuhudumia wananchi.

Mvutano wa uongozi Nairobi kati ya Gavana Mike Sonko na Meja Badi umekuwa ukishuhudiwa tangu kuzinduliwa kwa NMS, Sonko akilalamikia kudunishwa na shirika hilo.

Bw Sonko hata hivyo mnamo Jumanne alijitokeza na kuorodhesha listi ya miradi ya maendeleo aliyofanya tangu kuchaguliwa gavana wa Nairobi, huku akiitaka afisi ya NMS kumheshimu kama gavana.

Bila kuwataja kwa majina, gavana huyo alicharura baadhi ya viongozi wakuu serikalini akisema wanaendesha siasa potovu badala ya kuhudumia umma.

Katika hafla ya Jumatano kujadili huduma za maendeleo Nairobi, Rais Kenyatta ameyarejelea maneno ya Sonko akisema: “Jana (Jumanne) gavana Sonko alitueleza tukome kufanya siasa na badala yake tuwahudumie wananchi.”

Ukosefu wa maji jijini Nairobi na viunga vyake umekuwa kero kuu kwa wakazi, wenyeji wakiendelea kulalamikia uhaba wa raslimali hii muhimu.

Mtandao wa mabwanyenye umetajwa kushika mateka kampuni ya usambazaji maji Nairobi kwa manufaa yao binafsi.

Ukizuru mitaa kama vile Kariobangi, Mathare, Kibra, Mwiki, Kasarani, miongoni mwa mingine, uuzaji wa maji kwa malori na mikokoeni ndiyo tasira itakayokulaki.