Makala

HILLARY OWINO: Nalenga kuwa mwigizaji mahiri duniani

January 24th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

PENYE nia pana njia, ndivyo wahenga walivyologa. Tangia zama zile baada ya kupasua hilo mpaka sasa, msemo huo ungali na mashiko sio haba miongoni mwa jamii kwa jumla.

Pia inazidi kuthibitishwa na chipukizi wengi wanaozidi kushangamkia shughuli tofauti kwenye jitihada za kusaka riziki.

“Tangu nikiwa mdogo nilitamani sana kuhitimu kuwa mhandisi ingawa pia nilivutiwa na masuala ya maigizo,” anasema Hillary Omondi Owino lakini anaongeza kuwa jinsi maisha yalivyosonga mambo yalimwendea mrama. Kijana huyu anajivunia kuwa mwelekezi pia mpiga picha za filamu.

Chipukizi huyu alianza kujituma kwenye masuala ya maigizo mwaka 2017 alipojiunga na kundi la uigizaji lililofahamika kama Alphar’s Ferture is now lililopatikana katika Kaunti ya Kiambu.

Owino anasema kuwa kipindi hicho alifanikiwa kushiriki filamu nne chini ya kundi hilo zilizopata mpenyo na kupeperushwa kupitia Mt Kenya TV.

Katika mpango mzima anataka kukuza talanta yake akilenga kufikia kiwango cha waigizaji mahiri duniani kama Michael Gerard Tyson maarufu Mike Tyson ambaye wakati mmoja alikuwa bingwa wa masumbwi duniani. Bingwa huyo ameshiriki filamu kama ‘The Hangover (2017),’ na ‘Grudge Match,’ kati ya zingine.

Anadokeza kuwa analenga kufikia upeo wa kimataifa ili kuwa mfano mzuri kwa wanamaigizo chipukizi nchini. Ingawa anaamini sanaa ya maigizo inalipa anasema bado hajafanikiwa kuonja utamu wa malipo ya jasho lake maana hawajapata dili nzuri.

”Vyombo vya habari nchini vinastahili kuanzisha programu nyingi za kuonyesha filamu za wazalendo ili kutangaza utamaduni wetu. ”

”Pia wasanii wa humu nchini tunastahili kuwa mstari wa mbele kuzalisha filamu nzuri pia zinazogusa utamadumi wetu kama ilivyo kwa wanamaigizo wengine katika mataifa yanayoendelea katika tasnia ya uigizaji kama Afrika Kusini, Nigeria na Tanzania kati ya mengine.”

Chini ya kampuni ya Heart Media Services chipukizi huyu hufanya kazi kama naibu mwelekezi wa filamu ambapo husaidiana na John Kariuki pia mpiga picha katika harakati za kuzalisha filamu ya TV Series ‘Game Changer’. Filamu hiyo hupeperushwa kila wiki kupitia UTV.

Ingawa hajapata mashiko katika burudani ya uigizaji anadai bado anawazia kumiliki brandi yake ili kusaidia waigizaji chipukizi. Hata hivyo anasema mtaji umeibuka donda sugu kwenye juhudi za kutimiza ndoto yake.

Anatoa mwito kwa serikali angalau iweke mikakati mwafaka ili wasanii wanaokuja kwenye gemu wapate nafasi kukuza talanta zao.

Anashauri chipukizi wenzake wajiamini kwa vipaji vyao pia wajitume bila kulegeza kamba kwenye jitihada za kupapalia talanta zao.

Pia anawahimiza kuwa kando na changamoto nyingi zinazokuba sekta ya maigizo kamwe wasikate tamaa. Kadhalika anatoa mwito kwa wazazi wasiwe wanawafungia wanao wanajihisi wanacho kipaji katika uigizaji. Anasema mwanzo wanapaswa kuwapa nafasi na kufuatilia shughuli wanazojihusisha nazo.