Michezo

Hilton mwanasoka mkongwe zaidi kuchezea Ligue 1 akiwa na miaka 64

September 17th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

NAHODHA wa Montpellier, Vitorino Hilton aliweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza baada ya miaka 64 mwenye umri wa zaidi ya miaka 43 kusakata soka ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Hii ni baada ya sogora huyo mkongwe kuwa sehemu ya kikosi cha Montpellier kilichowapepeta Olympique Lyon 2-1 mnamo Septemba 15, 2020.

Hata hivyo, alionyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa mechi hiyo kwa utovu wa nidhamu. Kosa lake lilichangia penalti iliyofungwa na fowadi wa zamani wa Manchester United, Memphis Depay katika dakika ya 82.

Hilton ambaye alifikisha umri wa miaka 43 mnamo Septemba 13, amekuwa akisakata soka barani Ulaya tangu 2002.

Mabao yote mawili ya Montpellier ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano jedwalini, yalifungwa na Teji Savanier katika dakika ya 38 na 59 mtawalia.

Ushindi kwa Lyon ungaliwakweza kileleni mwa jedwali la Ligue 1 ila wakajipata wakimaliza mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya kiungo Houssem Aouar anayehusishwa pakubwa na Arsenal kuonyeshwa kadi nyekundu kunako dakika ya 44 kwa hatia ya kumchezea visivyo kiungo Arnaund Souquet.

Kufurushwa kwa Hilton na Aouar kunamaanisha kwamba jumla ya kadi 20 za rangi nyekundu zimetolewa hadi kufikia sasa kwenye soka ya Ligue 1 tangu mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO