Habari Mseto

Himizo adhabu ya kiboko irejeshwe kukabili utundu shuleni

September 28th, 2020 2 min read

PIUS MAUNDU na MISHI GONGO

HUKU serikali ikitathmini kufungua shule maambukizi ya virusi vya corona yakipungua, walimu wakuu wameomba serikali kurudisha adhabu ya fimbo shuleni.

Mkuu wa chama cha wakuu wa shule za msingi nchini (Kepsha), eneo la Masongale, Kaunti ya Makueni, Bw Joel Mathang’a, alisema likizo ndefu iliyosababishwa na janga la corona imefanya wanafunzi kujifunza tabia mbaya kwa kutangamana na waliopotoka kimaadili mtaani.

“Kurudisha nidhamu kwa wanafunzi waliojifundisha tabia mbaya katika likizo, ni lazima serikali iwaruhusu walimu kuwachapa wanafunzi hao shule zitakapofunguliwa,” akasema Bw Mathang’a, mwalimu kuu katika shule ya msingi ya Makutano.

Hata hivyo, mkurugenzi wa elimu katika kaunti ndogo ya Kibwezi, aliwaonya walimu watakaowaadhibu watoto kwa fimbo pindi shule zitakapofunguliwa akisema kuwa adhabu ya fimbo shuleni bado ni hatia.

“Likizo ndefu ambayo wanafunzi wamekuwa nayo ilikuwa muda muafaka kwa wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanadumisha nidhamu ya hali ya juu,” akasema Bw ….Machora.

Waliyasema hayo siku ya Jumamosi walipokuwa katika soko la Ulilinzi, ambapo mkazi mmoja Bw Festus Mwaniki alitoa ufadhili wa vifaa 180 vya kuosha mikono kwa wanafunzi kama njia ya kuhakikisha kuwa shule zinafuatilia masharti yaliyowekwa na wizara ya afya ya kujikinga dhidi ya corona shule zitakapofunguliwa.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na mwenyekiti wa chuo cha kutoa mafunzo ya udaktari, Bw Philip Kaloki, ambae aliwasisitizia Wakenya kutolegeza kamba katika kutekeleza masharti yaliyowekwa na wizara ya afya kupambana na ugonjwa wa Covid 19.

Kwingineko, katika Kaunti ya Mombasa, afisa mkuu, Bw John Musavu, alisema kuwa walimu wako tayari kurudi shuleni.

Alisema kaunti hiyo inaendeleza zoezi la kuzuru shule zote kuhakikisha kuwa zimetimiza vigezo vilivyowekwa na wizara ya afya.

“Tuko na kundi la maafisa katika sekta hii ambao wanatembea kwa shule kuzikagua jinsi zilivyojitayarisha kupokea wanafunzi wakitumia stakabadhi zilizotolewa na wizara ya afya,” akasema Bw Musavu.

Alisema sehemu ambazo hazina maji atahakikisha kumechimbwa visima. Pia alieleza kuwa amewasiliana na wanafunzi na hakuna aliyeambukizwa virusi vya corona.

“Tunafanya kazi kwa ukaribu na idara ya afya kuhakikisha kuwa walimu na wanafunzi wote wanapata ushauri nasaha shule zitakapofunguliwa,” akasema.

Wanafunzi watatumia ukumbi wa maankuli, vyandarua na madarasa kuhakikisha kuwa wana nafasi ya kutosha kuweza kudumisha umbali wa mita 1.5.

Aliongezea kuwa kuna baadhi ambao watahudhuria asubuhi na wengine mchana kuhakikisha kuwa hawakaribiani.

Naye mkurugenzi wa Elimu, Bw Moses Makori, alisema kaunti hiyo iko tayari kufungua shule japo wanakumbwa na changamoto ya nafasi za kutosha.

Mjumbe wa Chama cha Walimu cha Kitaifa (KNUT), eneo la Pwani, Bw Dan Oloo, aliwataka wazazi, walimu na wanafunzi kujitayarisha kwa ufunguzi wa shule.

“Janga la corona liliathiri dunia nzima, hatuwezi kuuliza mzazi mmoja mmoja kama wako tayari kurudisha watoto shule. Tunaelewa kuna wale walioachishwa kazi lakini Januari ikifika iwe pia hawajakuwa tayari kiuchumi? Tunachoomba ni serikali kuweka mikakati itakayowakinga wazazi na walimu,” akaeleza.