Habari

Himizo wabunge waunge mageuzi katika sekta ya majanichai

December 14th, 2020 2 min read

Na VITALIS KIMUTAI

WABUNGE kutoka maeneo yanayokuzwa majanichai nchini, wamehimizwa kuunga mkono mapendekezo yaliyotolewa kuifanyia mageuzi sekta hiyo, ili kuwalinda wakulima dhidi ya kukandamizwa na baadhi ya wadau.

Naibu Waziri katika Wizara ya Mafuta na Madini, Bw John Mosonik, alisema kuwa wabunge wanapaswa kuunga mkono mapendekezo hayo ili kuwawezesha wakulima wadogo wadogo kuanza kupata faida.

Hii ni baada ya wengi wao kulalamika kuhusu kukandamizwa na baadhi ya watu wenye ushawishi wanaoisimamia sekta hiyo.

“Wabunge kutoka maeneo hayo hawapaswi kuachwa nyuma mdahalo huo unapoendelea. Wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha hatua ya serikali kuwaondoa mawakala ambao wamekuwa wakiwapunja wakulima kwa muda mrefu imefaulu,” akasema.

Akiongea Jumapili kwenye hafla ya ibada katika kanisa la Chepsetion African Inland Church (AIC), eneobunge la Ainamoi, Kaunti ya Kericho, Bw Mosonik alisema inasikitisha kuwa licha ya majanichai kuwa miongoni mwa mazao yanayoipatia Kenya mapato ya juu kutoka nje, wakulima wadogo wamekuwa wakikandamizwa na Halmashauri ya Kusimamia Majanichai Kenya (KTDA) na sekta ya kibinafsi.

“Inasikitisha kwamba licha ya kazi nyingi wanazofanya, wakulima huwa wanalipwa kiwango cha chini sana kwa kilo moja ya majanichai wanayowasilisha kwenye viwanda. Kiwango hicho hata ni chini ya malipo ambayo vibarua wanaochuma zao hilo hupata. Katika hali hiyo, wengi hushindwa kukidhi mahitaji ya kimsingi ya familia zao kama matibabu, chakula na karo,” akasema.

Kiwastani, vibarua wanaochuma majanichai huwa wanalipwa Sh8 kwa kilo moja wanayochuma huku wakulima wakinunuliwa kiwango kama hicho Sh16, wanapowasilisha kwa KTDA na viwanda vya kibinafsi.

Hilo linamaanisha wakulima huwa wanapata kiwango sawa na vibarua wao.

Isitoshe, KTDA huwa inatoa malipo fulani kutoka kwa wakulima ambayo huwalipa kila mwisho wa mwaka kama bonasi.

Wakulima pia wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa ujenzi na ukarabati wa viwanda vinavyosimamiwa na halmashauri hiyo.

Ada zingine ambazo huwa wanatozwa ni kuhusu mbolea zinazosambazwa kwao na taasisi hiyo.

Kwa mpangilio huo, wengi walisema huwa hawapati faida hata kidogo.

Kwenye mapendekezo yaliyotolewa na Waziri wa Kilimo Peter Munya, serikali inalenga kupunguza idadi ya wakurugenzi kwenye viwanda vinavyosimamiwa na halmashauri.

Vile vile, viongozi katika viwanda hivyo watakuwa wakichaguliwa kwa mfumo wa kura moja kwa mkulima mmoja, kinyume na sasa ambapo wakulima hupiga kuwa kulingana na kiwango cha hisa wanazomiliki katika kiwanda husika.

Mapendekezo pia yanalenga kuhakikisha viwanda vina makatibu wao kinyume na sasa ambapo viwanda vyote 56 nchini vina katibu mmoja pekee.