Habari

Himizo Waislamu watii masharti hata wakati wa sherehe za Eid al-Fitr

May 20th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

VIONGOZI wa dini ya Kiislamu wamewashauri waumini wazingatie sheria na kanuni zilizowekwa kudhibiti virusi vya corona hata wakati wa sherehe za Idi yaani Idd ul-Fitri au Eid al-Fitr.

Sherehe hizo zinatarajiwa ziwe ama siku ya Jumamosi au Jumapili lakini hili linategemea na kuonekana kwa mwezi.

Akizungumza na Taifa Leo mwenyekiti wa kitaifa wa Baraza la Kitaifa la Ushauri kwa Waislamu (KEMNAC) Sheikh Juma Ngao, amewasihi Waislamu kutopuuza maagizo ili kujilinda na kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

“Ni sikukuu muhimu kwa waumini wa dini ya Kiislamu, lakini tunafaa kufuata sheria na masharti yaliyowekwa na serikali kupitia Wizara ya Afya na amri ya Rais,” amesema Sheikh Ngao.

Amewashauri waumini watekeleza swala zao nyumbani na pia waepuke kutembeleana ijapokuwa si mazoea yao.

Sikukuu ya Idi huashiria kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao huwa siku 29 au 30.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiangi ametangaza Jumatano kwamba mapumziko ya sikukuu hiyo ni Jumatatu, Mei 25, 2020.

Kwa kawaida Waisilamu kote nchini huadhimisha sikukuu hiyo kwa swala ya Idi inayotekelezwa asubuhi baada ya kuchomoza kwa jua. Hata hivyo, mwaka huu hakutakuwa na swala hiyo ya jumuiya kufuatia amri ya kutokongamana iliyotolewa na serikali.

Baadaye Waislamu hushiriki katika shughuli mbalimbali zikiwemo kutembelea marafiki na jamaa au sehemu za burudani.

Sherehe hizo huhusisha kupeana zawadi na kula pamoja na ndugu na marafiki.

Hata hivyo, mwaka huu sherehe hizo zitakuwa tofauti kufuatia masharti yaliyowekwa kukabili ugonjwa wa Covid-19.

Bi Salma Issac ambaye ni mkazi wa Mji wa Kale amesema kufikia sasa hajawanunulia wanawe nguo kama ilivyo ada kutokana na kufungwa kwa soko la Marikiti.

“Wakati kama huu huwa tayari nimeshawanunulia wanangu watatu nguo; tayari kwa sikukuu lakini mwaka huu mambo ni tofauti,” amesema.

Aghalabu hii itakuwa Idi ya kwanza kusherehekewa bila burudani katika maeneo ya umma.