Habari Mseto

Himizo watu watumie nguvu za umeme kufanya mapishi

March 25th, 2024 1 min read

NA SIAGO CECE

KWA muda mrefu, Wakenya wengi wamekuwa wakitumia kuni, makaa na gesi kupikia huku, wachache wakitumia vifaa vya umeme.

Lakini kampuni ya kusambaza nguvu za umeme nchini, ndiyo Kenya Power sasa inapendekeza wananchi kutumia umeme ili kusaidia kuhifadhi mazingira, na hivyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza eneo la Diani, Meneja wa Kenya Power Kanda ya Pwani Phineas Marete alisema kupika kwa kutumia nguvu za umeme kutakabili uharibifu wa mazingira, ikilinganishwa na gesi, makaa au kuni.

“Tunahimiza Wakenya kutumia stima kupika kwa sababu bei yake ni nafuu ukilinganishwa na njia zingine. Tukizidi kutumia njia hii pia tutapunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na kukata miti ya kuchoma makaa,” Bw Marete alisema.

Kulingana naye, watu wengi wamekuwa wakidhani kuwa mtu anapopika kwa kutumia umeme, matumizi yake yanaongezeka, lakini alieleza kuwa bei yake iko chini ikilinganishwa na kununua makaa.

Wakenya wengi wanaotumia makaa hununua kutoka kwa wauzaji wanaokata miti.

Bw Marete alisema kuna vifaa maalum vya kupikia kwa kutumia umeme ambavyo wasionavyo watahitaji kuvinunua.

Tayari, kuna baadhi ya Wakenya ambao wanatumia vifaa hivyo kupikia, na meneja huyo alisema anashirikiana na kampuni zinazouza bidhaa hizo ili ziuzwe kwa bei nafuu na kuongeza muda wa malipo ili mtu yeyote awe anaweza kununua.

Haya yanajiri huku Wakenya wakiomba Kenya Power kupunguza visa vya stima kupotea.

Lawrence Mwangi, mkazi wa Diani alisema kuwa kukatika kwa umeme mara kwa mara kunachochea mtu asitumie jiko la umeme kufanya mapishi.

Alieleza kuwa wakati mwingi wafanyibiashara wengi hupata hasara stima zinapopotea muda mrefu.

Wakati huo huo, wakazi walisema kampuni ya Kenya Power inapaswa kupunguza gharama ya kununua umeme kabla kuanza kueneza kampeni ya mapishi kupitia stima.