Habari MsetoSiasa

Hisia mseto kuhusu habari kwamba wabunge 17 wana virusi vya corona

April 9th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HABARI kwamba vikao vya Bunge la Kitaifa na Seneti wiki hii vilifutiliwa mbali baada ya kubainika kuwa baadhi yao wabunge na maseneta wameambukizwa virusi vya corona imeibua hisia mseto mwao.

Duru zilisema kuwa Wizara ya Afya iliwashauri Maspika Justin Muturi (Bunge la Kitaifa) na Kenneth Lusaka (Seneti) kufutilia mbali vikao hivyo ili kuzuia maambukizi zaidi miongoni mwa wajumbe hao  na wahudumu wa bunge.

Ilidaiwa kuwa kati ya wabunge 50 waliofanyikwa uchunguzi wiki jana, imebainika kuwa 17 walipatikana na virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Jumatano, Mbunge wa Gatundu Moses Kuria alimtaka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutoa ufafanuzi kuhusu madai kuwa baadhi ya wabunge na maseneta wanaugua ugonjwa huo.

Bw Kuria alimtaka Waziri Kagwe kutaja majina ya wabunge hao.

“Ikiwa ni kweli kwamba wabunge 17 walipatikana na virusi vya corona, Waziri Mutahi Kagwe anapaswa kutaja majina yao ili Wakenya ambao huenda wametangamana nao waende kupimwa,” akasema jana alipohojiwa katika redio moja jana asubuhi.

Bw Kuria aliongeza wabunge wanaweza kuwaambukiza watu wengi virusi hivyo ikizingatiwa kuwa wao hutangamana na watu kila mara. “Ikiwa kweli kwamba wabunge 17 wana virusi vya corona, basi huenda wameambukiza zaidi ya watu 50,000 ikizingatiwa kuwa mbunge anaweza kutangamana na zaidi ya watu 3,000 kwa siku chache,” akasema.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior aliungama kuwa wiki jana wabunge na maseneta walifanyiwa uchunguzi, kwa hiari, katika majengo ya bunge na maafisa kutoka Wizara ya Afya.

“Lakini matokeo yalitumwa moja kwa moja kwa kila mbunge na seneta. Binafsi sikupatikana na virusi hivyo. Kwa hivyo, siwezi kukana au kuthibitisha habari kwamba baadhi yetu walipatikana na virusi vya corona,” akaeleza Bw Kilonzo Junior ambaye ni kiranja wa wachache katika Seneti.

Mbunge wa Lugari Ayub Savula pia alisema ukweli kuhusu madai hayo yanaweza tu kutolewa na Wizara ya Afya au wabunge wenyewe.

“Kile ninachofahamu ni kwamba kikao cha maalum cha bunge la kitaifa kiliahirishwa kutokana na hali kwamba uongozi wa bunge haokuwa na uhakika kuhusu hali ya kiafya ya baadhi yetu. Lakini mimi binafsi niko salama,” akasema.

Japo Spika Muturi alipuuzilia madai  kwamba baadhi ya wabunge wamethibitishwa kuwa na Covid-19 na kuyataja kama uwongo, mwenzake wa Seneti Bw Lusaka alisema hangekana wala kuthibitisha madai hayo.

“Uchunguzi ulifanywa kwa hiari. Na madaktari hupeana matokeo kwa wabunge au maseneta husika kisiri. Ninaweza tu kuongea kuhusu hali yangu. Nilifanyiwa uchunguzi na nikapatikana kuwa salama,” akasema.

Majuma mawili yaliyopita wasiwasi ilishamiri miongoni mwa wabunge na wafanyakazi baada kubainika kuwa baadhi yao walitangamana na Mbunge wa Rabai Kamoti Mwamkale, ambaye alibainika kuwa na virusi hivyo.

Ilidaiwa kuwa Bw Mwamkale ambaye alikiri kuambukizwa baada ya kukutana na Naibu Gavana wa Kilifi Gideon Saburi, alihudhuria kikao cha pamoja na chama ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) na ile ya Kuchunguza Sheria Mbadala.

Mbunge huyo pia alidaiwa kuhudhuria vikao cha bunge cha alasiri mnamo Machi 17, siku ambayo bunge liliahirisha vikao vyao kutokana na janga la corona.

Hii ndio maana wiki jana, Tume ya Huduma za Bunge (PSC) iliamuru kwamba wabunge, maseneta na wafanyakazi wa bunge wajitokeze wachunguzwe ili kubaini hali yao.