Hisia mseto za wabunge kuhusu hotuba ya Rais Ruto

Hisia mseto za wabunge kuhusu hotuba ya Rais Ruto

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wameibua hisia mseto kuhusu hotuba aliyotoa bungeni Rais William Ruto alipohutubia kikao cha pamoja cha bunge la kitaifa na lile la seneti mnamo Septemba 29, 2022.

Hotuba hiyo ambayo iliashiria kufunguliwa rasmi kwa kikao cha kwanza cha Bunge la 13, ilikuwa ni ya kwanza kwa Dkt Ruto kutoa bungeni tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tano wa Kenya mnamo Septemba 13.

Huku wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza wakimsifu Rais Ruto kwa kutoa hotuba fupi na iliyoangazia masuala yanayolenga kuinua uchumi ya nchi, wenzao wa Azimio la Umoja-One Kenya waliipuuzilia wakidai ilikuwa “fupi zaidi bila chochote cha maana kwa Wakenya.

Kwa mtazamo wangu, Rais Ruto ametoa hotuba nzuri japo fupi ilikilinganishwa na zile zilizotolewa na watangulizi wake. Kwa kuagiza wizara kupunguza bajeti zao ili kuokoa Sh300 bilioni, Rais alioondoa mzigo mabegani mwa Wakenya kufadhili bajeti ya sasa.

“Hii bila shaka aitawezesha fedha nyingi kuelekezwa katika mipango mingine ya kuboresha uchumi kama mpango wa utoaji mbolea ya bei nafuu kwa wakulima,” akasema Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba.

Kwa upande wake Seneta wa Baringo William Cheptumo alimsifu Rais Ruto kwa kupendekeza kubuniwa kwa Hazina Maalum itakayotengewa fedha za kufadhili mpango kukagua utendakazi wa serikali za Kaunti.

Seneta wa Baringo William Cheptumo alimsifu Rais Ruto kwa kupendekeza kubuniwa kwa Hazina Maalum itakayotengewa fedha za kufadhili mpango kukagua utendakazi wa serikali za Kaunti. PICHA | CHARLES WASONGA

Aidha, alimpongeza Rais kuwa kutetea kuendelea kuwepo kwa Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (CDF) kwa kupendekeza iwekwe ndani ya Katiba ili iendelee kupiga jeki maendeleo.

“Wazo za kubuniwa kwa hazina ya fedha zitakazotumiwa na maseneta kukagua utendakazi wa serikali za kaunti. Kwa mfano, katika mwaka huu wa kifedha serikali za kaunti zimetengewa jumla ya Sh370 bilioni ambazo matumizi yazo zinafaa kuchunguzwa,” akasema Bw Cheptumo ambaye alihudumu kama Mbunge wa Baringo Kaskazini kwa mihula mitatu.

Lakini kwa upande wao, wabunge Azimio kama vile Opiyo Wandayi (Ugunja), Junet Mohamed (Suna Mashariki), Sabina Chege (Mbunge Maalum) na maseneta Ledama Ole Kina (Narok) na Godfrey Osotsi (Vihiga) walikosoa hotuba ya Rais Ruto.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi akitoa kauli yake kuhusu hotuba ya Rais William Ruto mnamo Septemba 29, 2022. PICHA | CHARLES WASONGA

“Huu ni muhula wangu wa tatu nikihudumu kama Mbunge. Lakini hii ni hotuba fupi zaidi. Inaonekana kuwa hawakuwa na chochote cha maana kutuelezea. Namuona Rais anazungumza kama mtu ambayo yungali kwenye kampeni. Anawasuta wapinzani wake huku akitoa ahadi zingine nyingi,” akasema Bw Junet ambaye ni kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa.

Kwa upande wake, Bi Chege alisema Rais Ruto alifeli kuelezea Wakenya waziwazi jinsi atakavyotekeleza ahadi nyingi alizotoa wakati wa kampeni.

“Hotuba ya Rais ilikuwa fupi zaidi lakini iliyosheheni matarajio makubwa. Hata hivyo, hakuelezea peupe jinsi atakavyotekeleza ahadi nyingi alizotoa kwa Wakenya. Pili, anazungumzia marekebisho ya sheriia ya Hazina ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) ilihali ni juzi tu ambapo bunge hilo lilipitisha mabadlliko hayo chini ya uongozi wangu kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya,” akaeleza Bi Chege, ambaye zamani alihudumu kama Mbunge Mwakilishi wa Murang’a.

Kwa upande wake, Seneta Ole Kina alipinga pendekezo la Rais kwamba CDF iliendelee kuwepo akisema wajibu wa wabunge sio kuhusika katika matumizi ya fedha za maendeleo bali kufuatilia matumizi yazo.

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina atoa hisia zake kuhusu hotuba ya Rais William Ruto bungeni, Septemba 29, 2022. PICHA | CHARLES WASONGA

“Kazi ya wabunge ni kutunga sheria na kufuatilia matumizi ya fedha wakati wa utekelezaji wa miradi katika ngazi za kitaifa. Lakini kwa kuwapa hazina ya CDF hiyo ni sawa na wao kujitwika kazi ambayo sio yao. Kwa hivyo, Rais Ruto anafaa kuheshimu uamuzi wa Mahakama ya Upeo,” akasema seneta huyo wa Narok.

Naye Seneta Osotsi alisema hotuba ya Rais Ruto aliwavunja moyo Wakenya kwa kutoonyesha jinsi atapunguza gharama ya maisha.

“Tulimtarajia kuongea kuhusu mipango yake ya kupunguza gharama ya maisha. Kupunguza bei ya mbolea hakutoshi kwa sababu bei ya mafuta ingali juu zaidi ambayo inayeyusha afueni hiyo,” akasema.

“Pili, Rais hakuelezea mipango ambayo itasaidia Wakenya kuimarisha uwezo wao wa kuweka akiba. Mbona Mkenya aweke akiba ya zaidi ya Sh200 kwa mwezi ilhali wanazongwa na makali ya kiuchumi,” akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge baada ya hotuba ya Rais.

Kwa upande wake kiongozi wa wengi Opiyo Wandayi alisema hotuba ya Dkt Ruto ilifeli kwa kutoangazia jinsi serikali yake itapambana na ufisadi.

“Nchi hii inapoteza zaidi ya Sh600 bilioni kila mwaka kupitia ufisadi lakini inasikitisha kuwa Rais hakuguzi kero hii. Swali langu ni je, pesa za kutekeleza ajenda zake za maendeleo zitatoka wapi ikiwa mianya ya ufisadi haitazibwa?”, Mbunge huyo wa Ugunja akauli.

 

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Kelvin Nyakundi

NPSC yateua kaimu DCI kushikilia kazi ya George Kinoti...

T L