HabariKimataifa

Historia Kenya ikianza kuuza mafuta katika nchi za kigeni

August 26th, 2019 2 min read

PSCU Na ANTHONY KITIMO

KENYA Jumatatu iliweka historia ya kuwa taifa la kwanza Afrika Mashariki kujiunga na mataifa yanayouza mafuta duniani.

Hii ni baada ya meli iliyobeba shehena ya kwanza ya mapipa 200,000 ya mafuta yaliyochimbwa katika Kaunti ya Turkana, kung’oa nanga katika Bandari ya Mombasa ikielekea Uingereza.

Mafuta hayo yameuzwa kwa Sh1.2 bilioni, bei ambayo ni ya juu kuliko iliyokisiwa awali.

Meli hiyo kwa jina Celcius Riga iliondoka bandarini mwendo wa saa sita adhuhuri kwenye sherehe iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Nina furaha kuu nikisema kuwa safari ya Kenya kuuza mafuta na gesi katika nchi za kigeni imeanza. Hii ni alfajiri mpya kwa Kenya na mwanzo wa kipindi cha ustawi kwa Wakenya wote,” akasema Rais.

Akaongeza: “Tutahakikisha kuwa raslimali za Kenya zimetumika kwa njia yenye manufaa makubwa kwa kizazi cha sasa na wakati huo huo kuzilinda kwa ajili ya kizazi kijacho.”

Alisema Kenya imeonyesha ulimwengu kuwa iko na uwezo na vifaa vinavyohitajika kwa utoaji wa mafuta ya kuuzwa kibiashara.

Rais alisema hatua itakayofuata ni uchimbaji wa kiwango cha juu na usafirishaji kwa mabomba kutoka Lokichar katika Kaunti ya Turkana hadi Bandari ya Lamu.

Kiongozi wa nchi alisema tayari wakazi wa Turkana wameanza kunufaika kutokana na uchimbaji wa mafuta kupitia nafasi za kazi na huduma nyingine.

Alieleza kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa jamii zinazoishi maeneo yenye raslimali mbalimbali zinanufaika zaidi.

Wakati wa hafla hiyo ya jana, Rais aliwapongeza Wakenya 136 ambao wameajiriwa na kampuni ya meli ya Mediterranean Shipping Company (MSC) kazi ya ubaharia.

Alidokeza kuwa serikali imehakikisha mabaharia hao watakuwa wakipokea malipo ya juu ambapo atakayelipwa mshahara wa chini zaidi kwa mwezi atapokea Sh85,000.

Manufaa mengine ni tiketi ya ndege kuja nchini kwa ajili ya likizo ya kila mwaka, chakula, malazi, bima ya matibabu na mafunzo ya hadhi ya juu.

Rais Kenyatta aliwaomba viongozi wa Pwani wafikirie miradi mpya itakayofaidi wakazi badala ya kutegemea bandari ya Mombasa pekee.

“Leo ninaenda Japan kujadili jinsi Dongo Kundu itajengwa na itaweza kuajiri maelfu ya watu. Naomba tusitegemee bandari ya Mombasa kama kitega uchumi pekee kwani kuna mabadiliko mengi, hivyo basi tujifunze kubuni miradi mipya itakayofaidi wakazi,” akasema.