Michezo

HISTORIA: Liverpool timu ya kwanza kuzoa pointi zaidi ya 90 na kukosa ubingwa

May 12th, 2019 2 min read

LONDON, UINGEREZA

NA MASHIRIKA

MASHABIKI wa Liverpool Jumapili walitamaushwa na ushindi wa Man City wa 4-1 dhidi ya Brighton uliowapa ufalme wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa pointi 98.

Liverpool imefunga msimu kwa alama 97, na kuwa timu ya kwanza katika historia ya EPL kupata zaidi ya pointi 90 na kukosa ubingwa.

Kampeni za muhula huu zimeshuhudia ushindani mkali kati ya klabu mbili za kwanza na nne nyinginezo ambazo zimekuwa zikiwania nafasi mbili za ziada za kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa (UEFA) msimu ujao.

Kubwa zaidi ambalo wakufunzi Pep Guardiola na Jurgen Klopp wamefanikiwa kwalo, ni kuwapa mashabiki wa soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) burudani tosha na kitu kipya cha kufuatilia zaidi katika msimu ujao wa kipute hicho.

Katika msimu wake wa tatu uwanjani Etihad, Guardiola ambaye ni mzaliwa wa Uhispania amefaulu kuwachochea masogora wake wa Manchester City kupiga soka safi zaidi yenye pasi za uhakika kama walivyokuwa wakicheza Barcelona wakati mkufunzi huyo alipokuwa akidhibiti mikoba ya miamba hao wa soka ya Uhispania.

Chini ya Guardiola, Man-City kwa sasa wamedhihirisha kwamba wana uwezo wa kutandaza soka ya kuvutia katika michuano yote ya haiba kubwa ndani ya Uingereza na kwenye mapambano ya bara Ulaya (UEFA).

Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba huenda Man-City wakatawazwa mabingwa wa mataji matatu mwishoni mwa kampeni za muhula huu.

Mbali na kutwaa ubingwa wa EPL, Man-City wanapigiwa upatu wa kuwapepeta Watford mwishoni mwa mwezi huu na kunyanyua Kombe la FA.

Kwa kweli, hatima ya Liverpool na Man-City katika kivumbi cha EPL muhula huu imesalia mikononi mwao wenyewe tangu kipenga cha mwanzo wa kampeni hizo kupulizwa mnamo Agosti mwaka jana.

Mbali na Liverpool, hakuna timu yoyote nyingine katika EPL ambayo kwa sasa inacheza mpira wa kushambulia zaidi kama Man-City ya Guardiola.

Tottenham, Chelsea, Arsenal na Manchester City waliokuwa wawe wapinzani wao wakuu, wamekuwa wakisuasua pakubwa.

Ingawa Liverpool wameanika kiu ya kutoa ushindani mkali kwa wapinzani wao hawa wakuu hadi mwisho, vita vya ubabe kati ya Klopp na Guardiola vimechangia sana kukoleza ladha na utamu wa EPL kadri wawili hao wanavyopigania fursa ya kutawala kabisa soka ya Uingereza.

Hadi mwishoni mwa wiki jana, Liverpool na Man-City walikuwa wamebadilishana usukani wa EPL kwa mara 37 tangu mwanzo wa msimu huu kipulizwe.

Ingawa timu nyingi zikiwemo Arsenal na PSG zimejaribu sana kuiga mtindo wa kupiga pasi fupi kama ilivyosisitizwa na Guardiola ugani Camp Nou, makocha wa vikosi hivyo bado hawajafanikiwa kabisa kufikia kiwango cha mkufunzi huyo.