Historia ya Malindi kama mji wa kifahari Uswahilini

Historia ya Malindi kama mji wa kifahari Uswahilini

Na Hawa Ali

MALINDI ni mji wa Kenya kwenye pwani ya Bahari Hindi. Mji huu u kilomita 100 Kaskazini ya mji wa Mombasa kwenye karibu na mto Athi-Galana-Sabaki.

Malindi ndio mji mkubwa zaidi katika Kaunti ya Kilifi na ni kitovu muhimu cha utalii Pwani ya Kenya. Mji huu huhudumiwa na uwanja wa ndege na barabara kuu kati ya Mombasa na Lamu.

Malindi ni kati ya miji ya kale ya Waswahili. Mji huu unajulikana kuwepo tangu karne ya 13 kwenye mwambao uliojulikana kama ‘Azania ‘ tangu zamani za Waroma na Wagiriki wa Kale.

Kwa karne nyingi, Malindi ulikuwa mji muhimu wa Uswahilini ulioshindana na Mombasa katika kipaumbele pwani ya Afrika ya Mashariki.Mnamo mwaka wa 1498 Mreno Vasco da Gama alifika Malindi kutoka kusini katika safari yake ya kwanza ya kuelekea Bara Hindi.

Wareno walikuwa watangulizi wa mataifa mengine ya Ulaya katika kutafuta njia za kufanya biashara.Vasco da Gama aliwahi kushirikiana na sultani wa Malindi kwa kusaini mkataba wa biashara uliodumu mpaka mwisho wa kuwepo kwa Wareno Uswahilini.

Alipewa nahodha ya kumwongoza hadi Bara Hindi, akajenga nguzo ya kumbukumbu inayosimama hadi leo karibu na bandari ya wavuvi ya Malindi.

Nguzo hiyo inasimama hadi leo hii.Katika mwaka wa 1499, Wareno walianzisha kituo cha kibiashara mjini Malindi ambacho kilikuwa cha watu kupumzikia wakiwa njiani kuenda na kutoka India. Kanisa lilianza wakati huo.

Fort Jesus

Mnamo mwaka wa 1593, Wareno walihamisha kituo chao kutoka Malindi hadi Mombasa walikojenga Fort Jesus.Katika Uswahili mpya baada ya kufukuzwa kwa Wareno 1693, umuhimu wa Malindi uliendelea kushuka na mnamo 1800 ulisalia mahali pa pori na maghofu tu.Baadaye utawala wa Usultani wa Zanzibar ulifufua mji.

Familia za makabaila kutoka kisiwa hicho na kutoka Omani walipewa ardhi karibu na Malindi wakaanza kujenga nyumba upya na kulima mashamba ya mazao ya kuuza kama pamba.

Tangu mwaka wa 1888, Malindi pamoja na pwani ya Kenya ilikodishwa na Zanzibar kwa Uingereza na kuondoka katika utawala wa Sultani.

Utalii

Polepole mwambao mzuri wa Malindi umepata sifa kama mahali pa kupumzika tangu miaka ya 1920. Nafasi nzuri ya kuvua samaki wakubwa ilivutia watalii wenye pesa.

Mji huu ni maarufu hasa miongoni mwa watalii kutoka Italia ambao wamependa Malindi na kununua nyumba na kujenga hoteli kadhaa.

Majengo mengi ya jadi yapo hadi leo, ikiwa ni pamoja na Msikiti wa Juma, magofu ya Gedi (pia inajulikana kwa jina Gede) Kusini ya Malindi ni maarufu kwa watalii.

Malindi imeunda baraza la manispaa ikiwa na kata kumi na tatu zifuatazo: Barani, Ganda/ Mkaumoto, Gede , Gede Kaskazini, Gede Kusini, Kijiwetanga, Madunguni, Malimo, Malindi kati, Malindi Kaskazini, Maweni, Shella na mji wa Watamu.

You can share this post!

Safaricom ilichangia Sh557 bilioni kwa pato la taifa...

WANDERI KAMAU: Ughaibuni si mbinguni, huko pia kuna magumu