Hit Squad kuelekea Congo Ijumaa

Hit Squad kuelekea Congo Ijumaa

 NA CHARLES ONGADI

TIMU ya taifa ya ndondi ‘Hit Squad’ inatarajiwa kuondoka nchini siku ya ijumaa kwa mashindano ya Africa Zone 3 Championship nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mashindano haya yanatarajiwa kung’oa nanga Machi 20 jijini Kinshasa ambapo zaidi ya nchi 9 zinatarajiwa kushiriki.

Akizungumza na Taifa Leo Digitali kwa njia ya simu kutoka Nairobi, mkurugenzi wa mawasiliano wa Shirikisho la Ndondi Nchini (BFK) Duncun ‘ Sugar Ray ‘ Kuria amesema kikosi cha taifa kimejiandaa barabara kwa mashindano hayo.

Kuria ambaye ni mwamba wa zamani wa timu ya taifa katika uzito wa fly, amesema kwamba kikosi cha ‘ Hit Squad ‘ kitawakilisha na mabondia 16 katika mashindano haya.

“ Kuna uzani kama tatu ambazo tulichagua mabondia wawili wawili na wote watakuwa katika safari ya DRC, “ akathibitisha Kuria.

Mabondia waliongezeka ni katika uzani wa fly ambapo kuna bingwa wa taifa Shaffi ‘ Black Musli ‘ Bakari na David  Karanja.

Katika uzito wa lightwelter kuna Joseph Shigali na Victor Odhiambo huku uzito wa Middle ikiwa na Edwin Okong’o na George Cosby Ouma.

Ouma na Okong’o watang’ang’ania nafasi iliyowachwa na Rayton ‘ Boom Boom ‘ Okwiri aliyeamua kuendelea kushiriki mashindano ya ndondi za kulipwa.

Mabondia wengine wanaotarajiwa kupeperusha bendera ya taifa nchini DRC ni nahodha Nick ‘ Commander ‘ Okoth katika uzito wa unyoya na Martin ‘ Oda ‘ Oduor.

Katika uzito wa welter kuna Boniface Mogunde Maina huku Hezron Maganga Sabat akitarajiwa kuwakilisha katika uzito wa lightheavy huku Joshua Wasike akiwa katika uzito wa Heavy.

Elly Ajowi atazichapa katika uzani wa Superheavy iliyokuwa ikimilikiwa na Fredric ‘ McGregory ‘ Ramogi aliyechujwa kikosini.

Kwa upande wa akina dada yupo Christine Ongare katika uzani wa fly ambaye tayari amefuzu kushiriki Michezo ya Olympiki ya Tokyo Japan.

Stacy Ayoma atakuwa katika uzani wa lightwelter kuchukua nafasi ya Everlin ‘ Tracy ‘ Akinyi huku Elizabeth Akinyi akiwa katika uzani wa welter  naye Elizabeth Andiego akiwa katika uzani wa Middle.

Timu ya taifa imekuwa katika maandalizi ya takribani miezi minne katika ukumbi wa AV Fitness iliyoko Lavingtone, Nairobi chini ya wakufunzi Musa Benjamin akisaidiana na Dave Munuhe na John Waweru.

  • Tags

You can share this post!

Uchunguzi waanzishwa kufuatia kifo cha mfanyabiashara Thika

Kaunti ya Nyeri yalenga kuchanja wanabodaboda 2,000