Habari

Hitilafu yasababisha umeme kukatika maeneo mbalimbali nchini

May 9th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SHUGHULI za biashara na huduma muhimu nchini zinazotegemea nguvu za umeme zimetatizika kwa muda wa zaidi ya saa sita ulipokatika kufuatia hitilafu ya kimitambo katika kituo cha kitaifa cha kuzisambaza.

Ni hali inayoshuhudiwa kote nchini, kampuni ya usambazaji stima, Kenya Power, kwenye notisi yake mapema Jumamosi ikiarifu kwamba mtambo wa kitaifa kusambaza nguvu za umeme ulipata hitilafu mwendo wa saa kumi na moja na dakika arubaini na tisa.

“Mafundi wetu wanaendelea kukagua mitambo kubaini shida ilipo na kuitatua,” Kenya Power ikaeleza. 

Biashara na viwanda visivyo na jenereta, ndizo huhangaika pakubwa na hali kama hii,

Vituo vingi vinavyotoa huduma za kimsingi kama vile hospitali, benki na hata vyombo vya habari mara nyingi huwa na majenereta kupiga jeki shughuli za kikazi.

Wanaohifadhi bidhaa za kula kwenye majokofu, huenda wakakadiria hasara vyakula vyao kuharibika endapo hitilafu hiyo itachukua muda kutatua.

“Tunaomba radhi kwa wateja wetu. Tutafahamisha umma shughuli za kurekebisha mitambo zinavyoendelea,” Kenya Power imeeleza kwenye notisi.