Makala

Hivi Kate Actress amepata mpoa mwingine baada ya ndoa kuingia mdudu?

January 2nd, 2024 1 min read

NA RAJAB ZAWADI

WANASEMA lisemwalo lipo na kama halipo, basi lipo njiani laja.

Taarifa zinataarifu kuwa mwigizaji staa Kate Actress atakuwa amejipatia mpoa mwingine baada ya ndoa yake kwa mtengenezaji filamu Phil Karanja kuvunjika.

Juzi kati wazazi hao wakiwa kwenye sherehe ya binti yao wa pekee alipotimiza miaka minne, walionekana kuonyesha ile kemia yao safi walipokuwa wanandoa.

Wengi wakaanza kuwashinikiza kwamba itakuwa vyema kama wakirejesha penzi lao. Hata hivyo, Kate aliweka wazi kuwa hilo haliweza kutokea.

Sasa taarifa zinadai kuwa hii ni kwa sababu Kate amekuwa kwenye mahusiano mapya kwa muda wa mwaka mmoja sasa na Meneja mkurugenzi Mkuu wa hoteli ya kifahari ya Tribe Hotel jijini Nairobi Michael Mwangi.

Wawili hao wamekuwa wakionekana kwenye viwanja mbalimbali wakila ujana. Wiki chache zilizopita walikuwa wote kwenye hafla ya kushuhudia sinema ya mchekeshaji Terrence Creative, Wash Wash 4 Icon. Kabla ya hapo walionekana kwenye shoo ya Sol Fest ambapo tiketi za VIP ziliuzwa kwa Sh20,000.

Juni 2023, wawili hao walionekana wakibangaiza na kula maisha visiwani Lamu.

Baadhi ya wadau katika hoteli ya Tribe Hotel wametuarifu kuwa ni kweli mahusiano ya bosi wao na mwigizaji huyo yamekuwepo kwa muda sasa.

“Umma unapata kujua sasa hivi ila wamekuwa pamoja kwa muda sasa. Kate mara nyingi alikuwa anafika hotelini huku kabla ya mahusiano yao kuanza,'” chanzo kimoja kilifichua.

Ndoa ya miaka sita ya Kate na Phil ilianza kuingia mdudu mwaka jana huku kukiwa na madai ya wawili hao kuchepukiana.

Jitihada zao za kujaribu kuficha msukosuko kwenye ndoa hiyo hazikufua dafu baada ya mapaparazi kuendelea kuwafuatilia kwa karibu sana.

Septemba 2023, wawili hao waliamua kuweka wazi kuwa ndoa yao tayari ilishavunjika na kila mmoja amkashika hamsini zake.