Bambika

Hivi kumbe mwimbaji wa injili kutoka Tanzania Christina Shusho ndio kiboko ya Gen Z wa Kenya?

April 3rd, 2024 2 min read

NA SINDA MATIKO

NDIVYO hivyo. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi majuzi kuelekea msimu wa Pasaka, kutoka kwa tuvuti ya kupakua muziki, Spotify, staa wa nyimbo za injili kutoka Tanzania, Christian Shusho ndiye msanii wa injili anayesikizwa sana hasa na kizazi cha Generation Z hapa nchini.

Shusho ameondokea kuwa kipenzi cha Wakenya na kilele chake kilishuhudiwa Novemba mwaka jana, alipotrendi kwa siku kadhaa kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani ukiitwa Twitter), wengi wakionekana kukoshwa na ubunifu wake wa kijanja kutumia maandiko ya Biblia kwenye  utungaji wa mashairi ya nyimbo zake.

Kwa kuona alivyokuwa akitrendi Kenya, Shusho akaitumia fursa hiyo kutangaza kwamba atapiga shoo Nairobi kwenye mkesha wa kuamkia Mwaka Mpya Disemba 31,2023.

Ni shoo ambayo ilifanikiwa pakubwa kwa kujaza mashabiki kweli kweli.

Lakini hata nje ya shoo, makali ya Shusho kwenye soko la muziki wa Kenya yanazidi kuonekana huku takwimu zikibeba ushahidi tosha.

Kwenye data ya hivi punde kuelekea Pasaka tuliyofanikiwa kuipata kutoka kwa Spotify, ni kwamba Shusho sasa amekita mizizi Kenya kwa kujitengenezea himaya mpya ya mashabiki ambao anaumiza vichwa vyao, kizazi cha Gen Z.

Nyimbo zake kadhaa haswa Shusha Nyavu inaongoza kwa usikilizwaji kwenye Spotify huku wasikilizaji wengi Wakenya wakiwa ni Gen Z.

Kando na Shusho, Gen Z Wakenya pia wameonyesha kuvutiwa na nyimbo za injili kutoka kwa wasanii kama vile Maverick City Music, Elevation Worship, Hillsong Worship na Chandler Moore kutoka Ulaya na Marekani.

Kwa mujibu wa data hiyo, toka 2022 hadi 2024, kumekuwa na ongezeko wa upakuaji wa miziki ya injili kwa asilimia 365% miongoni mwa Gen Z hapa nchini.

Aidha, pia podkasti za injili zimeonyesha kuanza kupata umaarufu Kenya, data hiyo ikiashiria ongezeko la 69% la usikilizwaji wa podkasti za namna hiyo kati ya 2022 hadi 2024.

Kwenye ripoti yao ya kila mwaka 2022, tovuti nyingine ya kupakua muziki Mdundo, iliripoti kuwa muziki wa injili ndio ulioongoza kwenye tovuti hiyo kwa kupakuliwa na kusikizwa zaidi Kenya.

Miziki ya injili iliongoza kwa asilimia 11%  ya usikilizaji ikifuatiwa na miziki kutoka Nigeria kwa asilimia tisa.