Habari Mseto

Hivi ndivyo tunavyoongezea kinga mwilini, asimulia Mkenya aliye Amerika

April 8th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Marekani inaongoza katika visa vya maambukizi ya virusi hatari vya corona vilivyoanzia mjini Wuhan nchini Uchina zaidi ya miezi mitatu iliyopita na kusambaa katika zaidi ya mataifa 200.

Mwandishi huyu alipata kuhoji mkaaji mmoja wa Marekani kuzungumzia jinsi alivyoathirika baada ya nchi hiyo kuripoti visa 339, 131 vya maambukizi na vifo 9, 689 kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo.

Roselyn Makani, ambaye ni mwalimu na dadake mwanamuziki maarufu mwendazake Ben Bahati, anaishi katika mji wa Little Rock, Arkansas, Marekani.

Amesimulia Taifa Leo hadithi yake ikiwemo kutaka watu watii sheria zinazolenga kupunguza maambukizi ya virusi hivyo pamoja na kufichua kuwa Wakenya wanaoishi Marekani wanakumbuka familia zao nchini Kenya na wana wasiwasi kuzihusu baada ya serikali kuthibitisha kuwa visa vimefika 158 na vifo sita Jumatatu.

“Mimi na familia yangu tunaendelea vyema hapa Marekani. Rafiki zangu ambao ni wauguzi wanafanya kila juhudi kushughulikia wagonjwa. Wana shughuli nyingi hata siwezi kuwafikia kwa njia ya simu.

Wengine wetu tunakaa nyumbani jinsi tulivyoagizwa na kuendelea kujiweka safi ili kuzuia kuenea kwa Covid-19. Mimi binafsi, nimepata motisha ya kuanzisha fomyula ya AMATUNDA LLC itakayosaidia kuinua kinga ya mwili ya watu wazee na watoto ili miili yao iweze kuwa na nguvu na tayari kupigana na virusi hivi.

Familia yangu imekuwa ikitumia fomyula hii, hasa watoto wangu wawili ambao nilipata kabla ya siku zao kufika na wamekuwa na matatizo ya upumuaji.

Fomyula hii imeimarisha kinga yao sana tangu waanze kuitumia. Nimeona matunda yake na kwa hivyo napanga sasa kufanya fomyula hii kuwa lishe maalumu na ninasubiri majibu ili nianze kutafuta fedha na kuufanya mradi.

Nasihi watu wasaidiane na kuombeana wakati huu mgumu. Naomba pia kila mtu atii sheria na kujitenga ili kuzuia uenezaji wa virusi hivyo.

Sisi kama walimu katika eneo letu tumeamua kufundisha wanafunzi wetu kupitia mtandao. Tunapatia wanafunzi wetu elimu kupitia apu ya Google Meet na kuwa na vikao vya walimu kupitia teknolojia ya Zoom.

Hatufundishi tu wanafunzi, lakini pia wazazi jinsi ya kupata mafundisho hayo kupitia huduma za Google Classroom na apu salama na rahisi ya kuwasiliana ya ClassDojo. Janga la virusi vya corona lilitupata kwa ghafla, lakini linafaa kuwa funzo kwetu na kila sekta.

Sisi kama Wakenya tunaoishi Marekani tuna wasiwasi kuhusu familia zetu nchini Kenya. Wakati huo huo, pia hatuna hofu kwa sababu tunajua watu wetu nchini Kenya tayari wamepitia mengi na kwa hivyo najua tutashinda vita hivi. Tunawasihi msikate tamaa na msiwe wachoyo. Saidianeni. Tuonyeshane upendo na fadhili. Tuonyeshe Ukenya ambao tunafahamika nao kote duniani.