Makala

Hizi ndizo sababu za baadhi ya wajawazito kutokwa na damu puani

December 11th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WANAWAKE wajawazito wanaweza kutokwa na damu puani si kwa sababu ni wagonjwa bali kutokana na mabadiliko ya homoni mwilini.

Wataalamu wanasema kuwa mwili wa mwanamke mjamzito hupitia mabadiliko tele.

Mabadiliko ya homoni yanaweza kumfanya kukokwa na damu puani, kulingana na Dkt Jordan Glicksman, mtaalamu wa upasuaji wa shingo na kichwa ambaye anachangia katika mtandao wa emedihealth.com ambao hutoa habari za afya.

Kadhalika, wakati wa ujauzito, damu nyingi huitajika kusaidia ukuaji wa mtoto tumboni.

Kuongezeka kwa kiwango cha damu inayopitia kwenye mishipa kunaweza kusababisha baadhi ya mishipa kupasuka.

Ili kujikinga na kuvuja kwa damu, mama mjamzito anashauriwa kutoachokonoa pua kwa kidole au kwa kutumia kitu chochote.

Kupenga kamasi mara kwa mara pia kunasababisha baadhi ya mishipa kupasuka hivyo damu kuvuja.

Kata kucha kuepuka kujeruhi pua wakati wa kupenga kamasi. Mambo ya kupotosha ambayo watu hufanya wanapotokwa na damu puani.

Watu wengi hufanya makosa kwa kuweka pamba au kipande cha nguo ili kuzuia damu kuvuja. Kufanya hivyo kunasababisha madhara zaidi na hakusaidii kwa lolote.

“Kosa jingine ambalo watu hufanya ni kulala chali wanapotokwa na damu puani. Kulala chali kunasababisha damu kuganda nyuma ya koo na tumboni, badala ya kuitoa nje,” anafafanua Dkt Glicksman.

Ni kosa pia kuinamisha kichwa huku ukikamua pua ili damu itoke haraka. Usiinamishe kichwa sana. Inamisha tu kidogo kuhakikisha kuwa inarudisha nyuma kasi ya damu kutoka.

Kulingana na Dkt Glicksman, mtu hashauriwi pia kuinamisha kichwa katikati ya miguu. Kuinamisha kichwa huleta presha puani hiyo kuongeza kasi ya damu kutoka.

Damu ikivuja sana mwathiriwa huenda akawa na maradhi ya anemia ambayo husababishwa na ukosefu wa damu mwilini.

Wataalamu wanashauri kuwa damu ikitoka kwa zaidi ya dakika 20 umwone daktari. Ikiwa mwathiriwa atapumua kwa shida pia anashauriwa kumwona mtaalamu wa matibabu.

“Ukianza kutapika damu kwa sababu ulimeza kiasi kikubwa, ni vyema kupata ushauri wa daktari. Damu ikitoka baada ya kujeruhiwa karibu na pua pia unafaa kumwona daktari,” anashauri daktari huyo.