Habari Mseto

Hofu BBI itarejesha rais mwenye mamlaka zaidi

October 25th, 2020 1 min read

Na WANDERI KAMAU

LICHA ya ahadi kuu ya ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) kuwa ingepunguza mamlaka makubwa ya rais kama ilivyo kwenye Katiba, imebainika kuwa mapendekezo ya ripoti hiyo yanairejesha nchi katika enzi ya ‘Rais Mfalme.’

Chini ya mapendekezo ya ripoti hiyo, mamlaka ya rais yanabaki kama yalivyo sasa, huku akiongezewa usemi mkubwa kuhusiana na nafasi mpya za waziri mkuu na manaibu wake wawili.

Ripoti hiyo inapendekeza rais awe akimteua waziri mkuu pamoja na mamlaka ya kumfuta kazi wakati wowote atakapo.

Hali ni sawa na hiyo kwa manaibu wake wawili, ambapo watakuwa wakiteuliwa na rais lakini anaweza pia kuwafuta kazi wakati wowote atakapo.

Ripoti hiyo pia inampa rais mamlaka ya kuwateua wanachama wa Afisi ya Kupokea Malalamishi ya Utendakazi katika Idara ya Sheria.

Hata hivyo, majina ya wale watakaoteuliwa kuhudumu katika afisi hiyo yataidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

Ikizingatiwa kuwa mamlaka mengi ya rais yanabaki yalivyo kama kiongozi wa serikali na mkuu wa majeshi, baadhi ya wanaharakati, wataalamu wa katiba na wadadisi wa siasa wanasema ripoti hiyo haitatoa tiba kwa baadhi ya maovu ya awali yaliyoshuhudiwa chini ya utawala wa chama cha Kanu.

Mwanaharakati Timothy Njoya anaitaja ripoti hiyo kuwa ‘maslahi binafsi’ ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Wadadisi wanasema kuwa chini ya mpangilio kama huo wa mamlaka, Kenya itakuwa sawa na ilivyokuwa katika miaka ya sitini, sabini na themanini, ambapo Kanu ndicho kilikuwa chama pekee cha siasa huku marais Mzee Jomo Kenyatta na marehemu Daniel Moi wakiwa wenye mamlaka makubwa.