Habari Mseto

Hofu corona ikizidi kusambaa shuleni, serikali ikisisitiza haitasitisha masomo

October 31st, 2020 2 min read

Na Waandishi Wetu

MAKALI ya virusi vya corona yanaendelea kutikisa shuleni wiki chache tu baada ya wanafunzi kurejea huku Kamusinga na Kimilili Boys’ zikiathirika. Ijumaa, wanafunzi 11 wa Kamusinga na sita wa Kimilikli walipatikana kuambukizwa virusi vya corona.

Wanafunzi wote sasa wametengwa mjini Webuye huku taharuki ikiendelea kutanda katika shule hizo ikishukiwa huenda wanafunzi wengine pia wameambukizwa corona.

“Wazazi wengi wamekuwa wakipiga simu huku wengine wakifika shuleni kuwajulia hali watoto wao. Tumehakikisha wanafunzi wote wanafuata sheria za Wizara ya Afya na pia wao huvaa barakoa, huketi umbali wa mita moja unusu na huosha mikono kila mara,” akasema Mwalimu wa Kamusinga ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mwalimu huyo alisema huenda shule hiyo ikafungwa kwa muda wa wiki mbili ili kunyunyizwe dawa ya kuua viini.

Katika Shule ya Upili ya Maranda, wanafunzi 10 walipatikana kuambukizwa. Hayo yalithibitishwa na Mkuu wa Afya katika Kaunti ya Siaya, Dkt Eunice Fwaya Hata hivyo, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alikiri serikali inapitia changamoto kuepusha wanafunzi kutagusana shuleni.

Licha ya hayo, alisisitiza shule hazitafungwa “hata kama kutakuwa na wimbi la tatu la maambukizi”.Kwingineko, aliyekuwa mwaniaji wa kiti cha ugavana wa Kakamega kupitia chama cha Jubilee, Bi Mable Muruli, jana aliaga dunia, familia yake ikithibitisha alikuwa na virusi vya corona.

Kwa mujibu wa nduguye Bw George Muruli, dadake aliaga dunia alipokuwa akihamishwa kutoka hospitali ya Coptic hadi ile ya Kenyatta. Marehemu pia amekuwa akisumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa moyo.“Jumapili iliyopita tulimpeleka hospitali ya Nairobi na mtaalamu wa magonjwa ya moyo akatushauri tumpeleke Coptic.

Alipimwa mnamo Jumatatu na akapatikana kuwa na virusi vya corona,” akasema Bw Muruli.“Alikabiliwa na matatizo ya kupumua na hali yake ikaendelea kudorora ndipo tukaambiwa tumpeleke hospitali ya Kenyatta Alhamisi usiku. Tulitafuta ambulensi ya kumhamisha lakini akafia njiani,” akaongeza.

Bi Muruli aliwania kiti cha ugavana kupitia Jubilee 2017 na akapoteza kwa gavana wa sasa Wycliffe Oparanya. Alipata kura 14,323 nyuma ya Boni Khalwale wa Ford Kenya (134,999) na Bw Oparanya (387, 999).

Kifo cha kiongozi huyo kinajiri chini ya saa 24 baada ya Mkuu wa wafanyakazi wa Kaunti ya Kakamega Robert Sumbi pia kufariki kutokana na virusi vya corona mnamo Alhamisi asubuhi.

Bw Sumbi alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahuti kwa siku tano kabla ya kuaga dunia.

Taarifa ya BRIAN OJAMAA, JUSTUS OCHIENG’, Ruth Mbula na Dickens Wasonga